Sambaza....

Baada ya Ligi kusimama kupisha michezo ya timu za Taifa kwa mujibu wa kalenda ya FIFA, Ligi Kuu Bara (TPL) inaendelea leo kwa michezo miwili. Azam fc watakua wageni wa Mwadui Shinyanga na African Lyon watakua wakiwakaribisha Wagosi wa kaya Coastal Union katika dimba la Uhuru.

Mchezo unaotarajiwa kuvuta hisia za wengi ni ule utakaowakutanisha  African Lyon na Coastal Union mchezo utakaopigwa katika dimba la Uhuru majira ya saa kumi kamili jioni. Mchezo huo utawakutanisha viungo wawili maswahiba na wachezaji wa zamani wa Simba na Taifa Stars. Ni Haruna Moshi “Boban” na Athumani Idd “Chujji” tena watakutana tena dimbani kuonyeshana ufundi.

Viungo hao waliotamba kwa wakati wao enzi zao wanategemewa kuiongezea mvuto mechi hiyo kutokana na uwezo wao pia uswahiba wao toka enzi wanacheza wote timu ya Taifa chini ya kocha Márcio Maximo!

Uwepo wa Alli Kiba kwa upande wa Coastal Union unaweza kuwavutia mashabiki pia lakini bado haiondoi utamu wa “battle” ya Boban na Chuji haswa kutokana na nafasi wanazocheza uwanjani. Boban anatumika kama namba 10 “Inside ten” nyuma ya mshambuliaji Victor da Costa huku Chujji akitumika kama kiungo mkabaji.

 

Sambaza....