Ligi Kuu

Kinachokosekana kwa Niyonzima kipo kwa Carlinhos

Sambaza....

Aliwahi kuitwa Fabregas wa Rwanda lakini mpaka sasa hivi ameshindwa kufanya vitu ambavyo Cesc Fabregas aliwahi kuvifanya kipindi ambacho alikuwa Arsenal , Barcelona na Chelsea.

Tulimpenda Cesc Fabregas kwa sababu alitumia muda mwingi kupika magoli kwa washambuliaji. Iliitwa habari ya kawaida kwa Cesc Fabregas kumaliza msimu akiwa na pasi zaidi ya kumi za magoli.

Ilikuwa kitu cha kawaida sana kushuhudia Cesc Fabregas akimaliza msimu akiwa na magoli zaidi ya kumi kwenye timu yake. Hii ndiyo ilikuwa sifa kubwa ya Cesc Fabregas . Atafunga na kutoa pasi za mwisho za goli.

Cesc Fabregas alikuwa na uwezo mkubwa wa kucheza mipira iliyokufa (faulo , kona na penalti). Alikuwa anaicheza kwa ufasaha mkubwa sana. Ufasaha ambao ulikuwa unasababisha magoli.

Cesc Fabregas alikuwa fundi haswa. Ufundi wake ulianza kufananishwa na Haruna Niyonzima , kiungo wa timu ya taifa ya Rwanda na klabu ya Yanga.

Wakati anakuja Yanga alipewa jina la Cesc Fabregas , miguu yake iliwavutia wengi na kuamini kwenye miguu yake kuna ufundi mkubwa kama ufundi aliokuwa nao Cesc Fabregas.


Hapana shaka hakuna ubishi kuwa Haruna Niyonzima anajua kuuchezea mpira. Macho yako yatatamani kila siku kuona miguu yake ikipata mpira kwa ajili ya ufundi wake.


Ufundi upo ndani ya miguu yake lakini kuna kitu kimoja ambacho kinakosekana kwenye miguu yake. Miguu yake haina macho kama ya Cesc Fabregas.

Haruna Niyonzima tangu aje Tanzania amefanikiwa kucheza misimu zaidi ya mitano lakini hakuna hata msimu mmoja ambao Haruna Niyonzima amemaliza akiwa na magoli zaidi ya kumi au pasi za mwisho za magoli zaidi ya kumi kama ambavyo Cesc Fabregas alivyokuwa anafanya.

Haruna Niyonzima siyo mzuri sana wa kupiga kwa ufasaha mipira iliyokufa. Mipira ambayo inaweza kuleta madhara makubwa kwa wapinzani kama faulo na kona.

Kitu hiki hakipo kwenye miguu yake , miguu isiyokuwa na macho. Wakati miguu ya Haruna Niyonzima ikiwa haina macho kuna miguu mipya ambayo imekuja Yanga.

Miguu hii ina macho. Miguu hii ni ya Carlinhos. Vitu ambavyo vinakosekana katika miguu ya Haruna Niyonzima vinapatikana kwenye miguu ya Carlinhos.

Carlinhos anauwezo mkubwa wa kucheza kwa ufasaha mipira iliyokufa kama faulo na kona. Carlinhos anauwezo mkubwa wa kutengeneza nafasi zaidi ya Haruna Niyonzima ndiyo maana nasema vitu ambavyo vinakosekana kwa Haruna Niyonzima vipo kwa Carlinhos.

Sambaza....