Ligi Kuu

KMC: Kuna burudani Kirumba, Simba ina wachezaji wazuri.

Sambaza....

Kikosi cha KMC FC kimefanya maandalizi yake ya mwisho leo kuelekea katika mchezo wa kesho wa Ligi kuu ya NBC soka Tanzania Bara dhidi ya Simba utakaochezwa saa 16: 00 jioni katika uwanja wa CCM Kirumba hapa Jijini Mwanza.

Timu hiyo ya Manispaa ya Kinondoni chini ya kocha Mkuu Thierry Hitimana imekamilisha maandalizi yake na kwamba ipo tayari kwa mtanange huo ambapo KMC FC ni mwenyeji wa mchezo huo.

KMC FC inatumia uwanja wa CCM Kirumba kama uwanja wa nyumbani kutokana na kanuni kutoa nafasi kwa vilabu kuchagua michezo miwili ambayo ingechezwa katika uwanja uliozoeleka na klabu husika kupeleka katika eneo ambalo wataona linafaa kwa mujibu kwa kanuni.

Kikosi hicho cha Wana Kino Boys ambacho kiliwasili Jijini Mwanza ijumaa usiku inakwenda kwenye mchezo huo ikiwa imetoka kushinda michezo miwili mfululizo katika uwanja wa Uhuru na hivyo kukusanya jumla ya alama sita muhimu na kufanikisha mpango wa kwanza wa mzunguko huo wa pili.

Katika mchezo huo, KMC FC inakwenda ikiwa na kumbukumbu ya kutoka sare ya magoli mawili kwa mawili kwenye mchezo wa mzunguko wa kwanza ambao ilikuwa ugenini katika uwanja wa Benjamini Mkapa.

Aidha KMC FC inatambua ushindani wa mchezo huo wa kesho kutokana na kila mmoja kuhitaji ushindi na kwamba kama timu imejipanga kuhakikisha kuwa inapata matokeo mazuri ili kuendelea kujiweka vizuri kwenye msimamo wa Ligi kuu ya NBC ambapo kwa sasa ipo kwenye nafasi ya tisa.

“Tunakwenda kwenye mchezo ambao utakuwa mgumu na ushindani kwa timu zote, ni mchezo ambao utakuwa na burudani kwa kila mmoja ambaye atakuwa amekuja kushuhudia, tuna waheshimu Simba kwasababu ni timu nzuri , inawachezaji wazuri lakini pia KMC FC ni timu bora na tunaamini kuwa tunauwezo mkubwa wakupambania alama tatu.” alisema Christina Mwagala, msemaji wa KMC.

Kwaupande wa Afya za wachezaji, KMC FC itawakosa nyota wake watatu muhimu ambao ni Hance Masoud Msonga, Emmanuel Mvuyekure pamoja na Matheo Anton lakini wengine wote wana hari na morali nzuri kwenye mchezo huo.


Sambaza....
Tafadhali tumia viungo vya mitandao ya jamii kusambaza.