Stori

Mbinu za Aussems zipo miguuni mwa Kagere na Mzamiru tu!

Sambaza....

Kila timu ina mchezaji ambaye ni muhimu sana katika kikosi. Umuhimu wa mchezaji katika kikosi hupimwa hasa kutokana na kazi yake uwanjani, jinsi anavyotumika katika kutimiza majukumu mbalimbali ya kimfumo na falsafa za kocha na klabu kwa ujumla.

Acha leo nikutembeza katika klabu ya Simba, ndani kabisa na huko tutaangazia mchezaji muhimu kabisa katika kikosi hicho katika mechi hizi 10 za awali ambazo klabu imezicheza kuanzia klabu bingwa Afrika hadi ligi kuu Tanzania

Meddie akiwa katika mazoezi

Kama ni mfuatiliaji mzuri wa klabu ya Simba utagundua kuwa kuna wachezaji ambao kila mechi lazima wacheze. Wachezaji hawa huwa ni lazima kucheza kwa sababu mbalimbali ikiwemo majeraha kwa wachezaji wengine pili ni mfumo wa Aussems unawafanya kufit vizuri na kuleta matokeo chanya.
Meddie Kagere na Mzamiru Yassin hawa ndio wachezaji wawili walionza michezo mingi zaidi katika klabu ya Simba. Wachezaji hawa kila mmoja ana sababu yake ya kuanzishwa kila mechi… Acha tuanze na meddie Kagere.

Kagere ameanza katika michezo yote ya klabu kuanzia klabu bingwa Afrika, mechi za kirafiki na ligi Tanzania bara. Katika kipindi chote hicho Kagere amekuwa akitumika kama Mshambuliaji wa mwisho huku akizunguukwa na viungo.

Kagere amekuwa akitumika katika mfumo wa 4-5-1, yeye husimama juu kabisa. Katika michezo yote Simba iliyocheza na mshambuliaji mmoja, imekuwa ikiiibuka na ushindi mwembamba na muda mwingine kufungwa kabisa. Mfano mchezo wa marudio dhidi ya UD- Songo na hata ule dhidi ya Mwadui FC, Simba iliambulia kipigo.

Pia katika mechi dhidi ya Azam ligi kuu, Simba ilipata ushindi mwembamba wa goli 1-0 lakini hakukuwa na nafasi nyingi za Kagere kufunga.
Kagere akitumiwa katika mfumo huu huwa anakabika kirahisi kwa sababu muda mwingi viungo wa Simba hujaa katikati na kuwafanya mabeki wa kati wa timu pinzani kumdhibiti kirahisi.

Katika mfumo huu, Aussems humtumia Kagere kama force 9 akiingia ndani kidogo ili kupunguza udhibiti wa timu pinzani na kuwaruhusu mawinga wa pembeni ambao mara nyingi huwa ni dilunga, kanda, Kahata au miraji kupita na kumuacha Kagere akiwa huru.Mfano ni goli alilofunga dhidi ya Azam.

Pili katika mfumo huu, Simba hutegemea mashambulizi ya aina tatu, kwanza ni kupitia kwa mabeki na mawinga, pili ni kupitia katikati, yaani Shiboub au Ajibu hutumika kutimiza mashambulizi haya, na mwisho kabisa ni mashambulizi ya kushtukiza, mfano ni mechi dhidi ya Azam, ngao ya JAMII goli la kahata na Chama ni matokeo ya shambulizi la kushtukiza katika mfumo wa 4-5-1.

Kagere pia amekuwa akitumika katika mfumo wa 4-3-3 ambapo yeye hucheza kama Central forward huku pembeni yake wakicheza washambuliaji wa pembeni ( Wing Forwards) wawili kama Miraji Athumani na ibrahimu Ajibu.

Katika mechi dhidi ya Mbeya City walicheza hivi na kupata ushindi Mnono wa goli 4-0. Pia dhidi ya Singida United walicheza hivyo na kushinda goli moja, uwanja ulionekana kuwa kikwazo pia.
Kucheza kwa aina hii, Simba huunda mashambulizi mengi kutokea pembeni, ambapo upande wa kushoto, miraji hukimbiza kwa kasi na kuingia ndani ya 18, huku ajibu akichezea katikati akitokea pembeni na kupiga kofi krosi.

Hadi hapa utakuwa umeshaelewa juu ya matumizi ya Miraji na Ajibu katika kumsaidia Kagere katika mfumo wa 4-3-3 kupachika magoli. Miraji huingia ndani akitokea pembeni kwa kasi, huku Ajibu huchezea katikakati na kutokea pembeni hii hufanya Kagere na Miraji kuwa standing striker wawili katikati na Ajibu kuwa Wing-forward na kutengeneza idadi ya wachezaji watatu wa Simba katika eneo la hatari la mpinzani timu inaposhambulia na wawili timu inaposhambuliwa.
Unaweza kujiuliza kwanini Kagere anatumika katika kila mfumo? Kuna sababu kuu mbili, moja ni ya nje ya uwanja na nyingine ni ya ndani ya uwanja.

Kwanza kabisa ni majeraha ya Washambuliaji wawili wa Simba kwa wakati mmoja, John Bocco na Wilker Da Silva. Hii humnyima Aussems nafasi pana ya kufanya uchaguzi wa Mshambuliaji yupi aanze. Kiufupi hana namna nyingine zaidi ya kuanza na Kagere.

Pili ni game intelligence ya Meddie Kagere mwenyewe. Hii inamaanisha kuwa Kagere mwenyewe anajimudu uwanjani, huenda hata kama Washambuliaji wengine wangekuwa fiti bado huenda angeanza kila mechi.

Game intelligence ni uwezo wa mchezaji kujua anatakiwa kuwa wapi kwa wakati gani uwanjani, mchezaji ajue timu inahitaji nini na yeye anatakiwa afanye nini, awe na nidhamu ya kiuchezaji ndani na hata nje ya uwanja hivi vyote vinamfanya Kagere awe chaguo la kwanza kwa Aussems.

Uwezo wake wa kucheka na nyavu, kasi, umiliki wa mpira, mashuti vyote vinafanya kuwa tishio kwa timu pinzani, hii huwapa nafasi wachezaji wengine kuwa huru na hata kufunga mabao, Sifa hizi zote zinamfanya kagere kutumika katika kila mfumo ili tu Simba iweze kupata ushindi.

Tuachane na Meddie Kagere sasa acha tumuangalie mchezaji wa pili na wa mwisho, Mzamiru Yasin.
Wengine wanapenda kumuita kiungo punda kwa maana ni kiungo anayetumika sana lakini mimi napenda kumuita kiungo- Mbweha.

Msimu uliopita Simba ilikuwa na viungo wa aina mbili, kwanza ni wale wazuri wakiwa na mpira mguuni kama Jonas Mkude na Said Ndemla, pili ni wale wazuri wakiwa hawana mpira kwa maana hawa walitumika zaidi katika kukaba pekee mfano ni James Kotei na Mzamiru Yassin,
Katika kundi la viungo hawa Aussems aliwatumia viungo wawili wenye sifa tofauti ili kutimiza majukumu kisahihi. Alimtumia Kotei kama mkabaji na mtibua mipango, na alimtumia Mkude kama mpiga pasi mpenyezo, hii inamaanaisha kuwa alikuwa na “stopper” (Kotei) na Muanzisha mashambulizi kuanzia nyuma (Mkude).

Jonas mkude akimnyanyasa kiungo wa Al-Ahly

Katika mfumo huu wa Aussems, Mzamiru alibaki nje kutokana na kutowafikia kiviwango wachezaji hawa wawili, yaani alikuwa mkabaji zaidi lakini pasi nyingi zilikuwa mbovu.

Mechi za mwishoni mwa Msimu, Mzamiru alianza kuimarika kitu kimoja baada ya kingine. Mabadiliko yake yalikuwa ni katika ukabaji na kupiga pasi. Tofauti na Zamani ambapo Mzamiru alikuwa mtenda Madhambi muda wote, alianza kupunguza hatari ya yeye kufanya madhambi akaanza kunyang’anya mipira bila kufanya madhambi, pili pasi zake zikaanza kuwa na macho.

Kuimarika kwake katika vitu hivi vichache vilimshtua Aussems kuwa Mzamiru akiimarika zaidi atakuwa ni mtamu zaidi ya kotei, na hii ndio sababu ya Kotei kutemwa Msimbazi bila hata kupepesa macho… Tuachane na Msimu uliopita acha tujikite katika msimu huu.

Mzamiru

Mechi ya Marudio dhidi ya UD Songo, Mzamiru alitokea benchi na kucheza vizuri kuisadia timu kupandisha mashambulizi, baada ya hapo mechi zote za ligi Mzamiru alianza.
Dhidi ya JKT Tanzania , Mtibwa Sugar, Kagera Sugar, Azam, na Mwadui, Mzamiru alianza na Fraga Vieira katika eneo la chini huku dhidi ya Biashara United na Singida United alianza na Said Ndemla.
Katika mechi zote, Mzamiru alicheza kama “BackUp” kwa maana alishuka chini kuwa kiungo wa ulinzi na kupanda katikati kama central Midfielder.

Alibadilishana maeneo ya kiulinzi na Fraga, katika kuhakikisha kuwa timu inabaki kuwa na mlingano sahihi kuanzia eneo la ulinzi hadi ushambuliaji.
Mzamiru ndio injini ya Simba kwa sasa katika eneo la kati, yeye hushuka chini kumsaidia kiungo wa ulinzi. Ukiitazama vizuri mikimbio ya Mzamiru utabaini kuwa, Mzamiru hukabia kushoto na kulia, hushuka chini zaidi kuwa kiungo wa ulinzi na akishambulia kupitia katikati hii humfanya kuunda umbo la “Diamond”. Mikimbio hii yote inamaanisha kuwa Mzamiru hufanya majukumu matatu uwanjani, Kwanza ni kumlinda kiungo chini, kuilinda safu ya Ulinzi na kushambulia kwa kupiga pasi mpenyezo za haraka na muda mwingine kushambulia mwenyewe kwa kukimbia na mpira kwa kasi huku akipiga vyenga.

Tofauti na Msimu uliopita Mzamiru wa sasa anajua kupiga vyenga, kukaba kwa nguvu na kasi, kukaba akitokea nyuma ( blind side defending), kupiga pasi za aina zote, ndefu, fupi, mpenyezo na kasi ya kukimbia na mpira kuelekea katika eneo la hatari.

Ubora wake mkubwa upo katika vipindi vya mpito. Simba inaposhambuliwa, Mzamiru huwa ndio mchezaji wa kwanza kuandaa mazingira ya mashambulizi ya kushtukiwa pindi wanapoupora mpira kutoka kwa maadui zao.

Kasi yake ya kukimbia na kupiga vyenga husaidia katika hili. Mzamiru huwa na mawasiliano ya Siri kati yake na Kagere hasa katika kipindi hiki cha mpito kutoka kushambuliwa kwenda kushambulia.
Kuna tofauti kubwa ya kiuchezaji kama Mzamiru akicheza juu ya Ndemla au Fraga. Akicheza na Fraga hushuka chini kama kiungo wa pili wa ulinzi . Akicheza na Ndemla hucheza kama Kiungo wa kati kuliko kiungo wa ulizi.Mzamiru pia anaweza kucheza kama kiungo wa ulinzi akiwa peke yake. Mfano katika mechi dhidi ya Mbeya City alicheza

Mzamiru kucheza kama kiungo wa ulinzi kuna masharti yake, nayo ni kuzunguukwa na viungo wengi. Kwa mfano katika mechi dhidi ya Mbeya City alizunguukwa na Shiboub, Chama na Ajibu. Hii inamaanisha kuwa jukumu la Mzamiru linakuwa ni moja tu nalo ni kuwa kiungo wa ulinzi.

Hadi kufikia hapo bila shaka utakuwa umenielewa nikikwambia kuwa Mzamiru ni Kiungo Mbweha. Anapewa majukumu mengi uwanjani lakini uwezo wake wa kuyatekeleza ni mkubwa kiasi cha kuwa mchezaji tegemeo ndani ya kikosi cha Aussems.

Twende sawa, niambie maoni yako ni yepi, Je unakubaliana na mimi kuwa Kagere na Mzamiru ndio wachezaji wakutumainiwa zaidi ndani ya Msimbazi?


Sambaza....
Tafadhali tumia viungo vya mitandao ya jamii kusambaza.