Blog

Miguu ya Pascal Wawa na Erasto Nyoni imepungua kasi

Sambaza....

Tuanzie hapa , unakumbuka ile Simba ya Patrick Aussems ? Simba ya msimu jana ambayo ilifanikiwa kufika hatua ya robo fainali ya ligi ya mabingwa barani Afrika ? Ile Simba ambayo ilishinda mechi zote za nyumbani kwenye mashindano hayo ya ligi ya mabingwa barani Afrika?

Nahisi unaikumbuka vyema , na kila mtu anaweza akawa na kitu ambacho kinaweza kumkumbusha kuhusiana na kikosi hicho. Kuna mwingine anaweza kukutajia ule utatu wa eneo la ushambuliaji, John Bocco , Emmanuel Okwi na Meddie Kagere.

Kwa bahati mbaya huo utatu haupo tena msimu huu baada ya Emmanuel Okwi kuondoka Simba . Tuachane na hili. Turudi kwenye kumbukumbu mbalimbali za kikosi cha Patrick Aussems cha msimu jana .

Kuna wengine wanaweza kumkumbuka James Kotei ambaye alikuwa pamoja na Swahiba wake Jonas Mkude katika eneo la kiungo cha kati. Eneo ambalo walifanya kazi ambayo ilikuwa kubwa sana na yenye kumbukumbu kubwa sana.

Kotei (Kushoto) akimthibiti Muleka wa TP Mazembe

Lakini akili yangu inawakumbuka Pascal Wawa na Erasto Nyoni . Mabeki imara wa kati , hawa walikuwa mhimili mkubwa sana kwenye majukumu ya kushambulia pamoja na kulinda. Tuanze na jukumu la kujilinda.

Walikuwa imara sana kuifanya safu yao ya ulinzi kuhakikisha iko dhabiti kuzuia hatari nyingi zinazokuja kwenye eneo lao. Kuna wakati pia walikuwa wanawapanga vyema hata viungo wa kati wakati timu yao ilipokuwa inashambuliwa.

Achana na jukumu lao la kuwapanga vyema mabeki na wachezaji wengine wakiwa kwenye eneo la kuzuia , lakini Pascal Wawa na Erasto Nyoni walikuwa imara zaidi kwenye miguu yao kupambana na washambuliaji mbalimbali kuhakikisha wanawazuia.

Walikuwa imara kuhakikisha kila mshambuliaji alikuwa akidhibitiwa kwa kiasi kikubwa, miguu yao pia ilikuwa imara zaidi kipindi timu yao inapoanza kushambulia, ndipo hapa umuhimu wao wa kushambulia unapoanzia.

Unaweza ukashangaa ninaposema walikuwa na mchango mkubwa sana wakati timu inaposhambulia . Patrick Aussems alikuwa na mtindo wa kuhakikisha timu inaanza kushambulia kwa kuanzia nyuma.

Mabeki wa kati ndiyo walikuwa na jukumu la kuanzia mashanbulizi kutokea nyuma. Pascal Wawa na Erasto Nyoni walikuwa wanakokota mipira na kupiga pasi kama viungo wa kati. Walikuwa na uwezo wa kupiga pasi ambazo zilikuwa zinaanzisha mashambulizi kwenye timu .

Wakati nilipokuwepo kwenye uwanja wa Taifa nikiwatazama Simba na Ruvu Shooting hapo jana nilikuja kugundua kuwa miguu ya Pascal Wawa na Erasto Nyoni siyo ile miguu ambayo walikuwa nayo wakati wa Patrick Aussems.

Pascal Wawa na Erasto Nyoni walikuwa hawana uwezo mkubwa wa kupambana na washambuliaji wa Ruvu Shooting kama ambavyo walikuwa awali , pia hata ule uwezo wa kuanzisha mashanbulizi umekuwa hafifu siyo kama ambavyo walivyokuwa msimu uliopita.

Sambaza....