Shirikisho Afrika

Ni Wawa au Mzamiru kesho!?

Sambaza....

Kuelekea katika mchezo wa robo fainali ya Kombel la Shirikisho Afrika dhidi ya Orlando Pirates Simba itawakosa wachezaji wake muhimu mlinzi wa kati Joash Onyango na kiungo Sadio Kanoute kutokana na adhabu ya kupata kadi 3 za njano.

Katika michezo sita ya hatua ya makundi waliyoshuka dimbani Kanoute na Onyango ndio nyota pekee waliopata adhabu hiyo ya kadi tatu za njano huku wengine kama Eransto Nyoni, Benard Morrison na Aishi Manula wakiwa na kadi moja ya njano.

Kuwakosa nyota hao wawili maana yake kunamfanya kocha Pablo kukuna kichwa na kupanga upya kikosi chake ili kuendana na mahitaji ya mchezo huo muhimu wa robo fainali.

Sadio Kanoute “Mkuki” akichukua mpira mbele ya wachezaji wa Asec Mimosa.

Pablo anakwenda kuwakosa nyota ambao wamekua katika kikosi cha kwanza katika michezo yote ya hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika isipokua Kanoute pekee alieukosa mchezo dhidi ya USGM kutokana na majeruhi.

Katika eneo la ulinzi ni wazi sasa Pablo anapaswa kumuandaa kati ya Pascal Wawa au Kenedy Juma ili kwenda kuziba pengo la Mkenya Joash Onyango ambae alikua akitengeneza ukuta na Inonga Baka.

Ni wazi huenda mlinzi mzoefu Pascal Wawa akachukua nafasi ya Joash Onyango mbele ya Kenedy Juma ili kwenda kuunda “partnership” na Henock Inonga Baka katika mchezo dhidi ya Orlando Pirates. Pascal Wawa licha ya kuonekana kushuka kwa uwezo wake siku za hivi karibuni lakini huenda akawa na faida ya uzoefu wa mechi kubwa kumzidi Kenedy Juma.

Joash Onyango

Pascal Wawa licha tu ya uzoefu lakini pia ni mtulivu anapokua na mpira haswa katika kuanzisha mashambulizi na upigaji wake wa mipira mirefu. Lakini sio mzuri sana katika mipira ya juu na kukosa kwake kasi kunamfanya kupata tabu mbele ya washambuliaji wasumbufu na wenye kasi.

Kenedy Juma amekua vyema katika kucheza mipira ya juu kutokana na kimo chake lakini sio mzuri katika kuituliza timu na kuanza kutoka na mpira kuanzia chini.

Kenedy Juma.

Katika eneo la kiungo kukosekana kwa Kanoute ni wazi sasa Thadeo Lwanga au Mzamiru Yassin watakua chaguo sahihi kwa Kocha Pablo Franco.
Kanoute amekua akijenga “partenership” nzuri na Jonas Mkude si tu katika michuano ya CAF lakini pia hata katika michezo ya NBC Premier League.

Thadeo Lwanga na Joash Onyango wakimdhibiti Nurkovic wa Kaizer Chiefs.


Nafasi kubwa yakuziba pengo la Sadio Kanoute inakwenda kwa Mzamiru Yassin ambae kwa kiasi kikubwa ana uzoefu na uwezo wakucheza mechi zenye uhitaji wa “intensity” ya hali ya juu kama hizi.

Ni wazi kukosa utimamu wa mwili katika mechi kwa asilimia mia moja kutamnyima nafasi Thadeo Lwanga mbele ya Mzamiru Yassin katika mchezo huo wa robo fainali.

Mzamiru Yasin.

Kocha Pablo kesho ana kibarua kigumu dhidi ya Orlando Pirates lakini pia ni wazi ana kibarua kingine cha kuchagua kati ya Pascal Wawa na Kenedy Juma kuziba pengo la Joash Onyango lakini pia Mzamiru Yassin au Thadeo Lwanga nani azibe pengo la Sadio Kanoute “Mkuki”.

Sambaza....