Mataifa Afrika

Obi kurejea timu ya Taifa kwa ajili ya AFCON.

Sambaza....

Kiungo John Obi Mikel amethibitisha kwamba ataitumikia timu ya Taifa ya Nigeria ‘Super Eagles’ kwenye fainali ya Mataifa Afrika zinazotarajiwa kufanyika kuanzia mwezi ujao nchini Misri.

Taarifa kutoka kwenye uongozi wa timu ya Taifa zimesema kwamba Mikel tayari ameshakutana na kocha Rohr Gernot nchini Uingereza kujadiliana na hilo na kuthibitisha kuwa ataitumikia timu hiyo kwa mara nyingine tena.

“Mikel amekutana na kocha Rohr nchini Uingereza na amethibitisha kuwa atakuwa miongoni mwa wachezaji wataoliwakilisha Taifa kwenye michuano ya Mataifa Afrika itakayofanyika nchini Misri,” taarifa hiyo imesema.

Kiungo huyo wa zamani wa Chelsea ambaye kwa sasa anaichezea Middlesborough hajaitumikia timu ya Taifa toka kumalizika kwa michuano ya Kombe la Dunia mwaka jana nchini Russia, na toka mwaka 2005 alipoanza kuitumikia timu hiyo dhidi ya Libya amefanikiwa kufunga mabao sita katika michezo 85.

Uzoefu wake na hulka ya uongozi aliyonayo ndiyo inayoonekana kumshawishi kocha kumjumuisha kwenye kikosi ambacho wachezaji wake wengi wanatarajiwa kuwa vijana ambao watakuwa ndo kwanza wanaanza kuitumikia timu ya Taifa.

Nigeria wapo kundi B pamoja na timu za Burundi, Madagascar na Guinea.


Sambaza....
Tafadhali tumia viungo vya mitandao ya jamii kusambaza.