Sambaza....

Tasnia ya michezo ilipatwa na msiba wa mchezaji nguli Athumani Juma “Chama” a.k.a Jogoo mlinzi mahiri aliyepata kuitumikia Dar Young Africans na Timu ya Taifa.

Nilikua nikitafuta muda wa kuelezea kwa ufupi umahiri wa huyu Marehemu wakati wa uhai wake, Athumani Juma alianzia Pamba ya Mwanza akihudumu kama beki wa pembeni na hata alipojiunga na Yanga mwaka 1981 alikua kitumika kama full back wa kulia kabla hajahamia kwenye nafasi iliyompa umaarufu ya Centre back.

Athumani Juma Chama alipata umaarufu zaidi East and Central Africa kwa umahiri wake wa kuwazuia wale vinara wa ufungaji kama vile Zamoyoni Mogella “Golden Boy” wa Tanzania na Ambrose Ayoyi aliyekuwa “Golden Boy” pale Kenya, Chama ndio alikua akipewa jukumu la kuwakabili wafumania nyavu wa timu yoyote pinzani na kweli hawakufurukuta, nakumbuka hata goli pekee ambalo Zamoyoni Mogella aliwafunga Yanga Athumani Juma alikua hajaanza kutumikia nafasi ya Centre Back.


Marehemu hakua mtu mkorofi kwenye uchezaji wake kama ambavyo tumewazoea wachezaji wengi mahiri wa zama zile ni mtu aliyekua akiwakabili wapinzani wake kwa kutumia akili nyingi na nguvu zake alizojaaliwa na Mwenyezi Mungu.

Marehemu Athumani Juma ‘Chama’ (katikati) akiwa na wachezaji chipukizi wa Yanga mwaka 1986, Athumani China (kulia) na Abubakar Salum ‘Sure Boy’ (kushoto)


Nje ya uwanja Marehemu alikua ni mpole na mcheshi, kitu ambacho wengi hawakukitaraji ni ule uhasama wake na Zamayoni Mogella ndani ya uwanja uliishia palepale tu baada ya zile dakika 90 nje ya hapo walikua ni marafiki wakubwa, niliwahi kuwashuhudia wakiwa pamoja mara kwa mara maeneo ya Mnazi Mmoja Primary kwenye miaka ya 1984 wakati huo nikiwa Mnazi Mmoja Primary, katika moja ya matukio ninayoyakumbuka kulikua na mwanafunzi mwenzetu alimtania Mogella kwa kumbeza kuwa yupo na Jogoo wake yule mwanafunzi aliambulia makonzi kutoka kwa wote wawili.

Zamoyoni Mogella kushoto, alikuwa rafiki mkubwa wa Chama nnje ya Uwanja ila Mahasimu uwanjani


Hata wakati akiugua Mogella alikua karibu sana na Marehemu katika kumfariji na kumpa misaada mbalimbali.
Hakuhudumu sana kwenye soka la Tanzania kwani 1985 alitimkia arabuni ( kumbuka ni miaka minne tu tangu amejiunga Yanga) aliporejea tena hakuwa Chama tuliyomzoea kwani tayari alikua na tatizo sugu lililokua likiwamaliza wachezaji wengi wa zama zile ugonjwa wa goti.


Pumzika kwa amani mwamba wa soka niliopata kuwashuhudia kwa macho yangu Athumani Juma Chama “Jogoo”
Mwenyezi Mungu akupe kauli thabit.

Mkubwa Kambi

 

Sambaza....