Kotei (Kushoto) akimthibiti Muleka wa TP Mazembe
Blog

Sababu 5 za kiufundi za kuachwa kwa James Kotei.

Sambaza kwa marafiki....

JAMES AGYEKUM KOTEI alijiunga na Simba mwaka 2016, akiwa kama kiungo wa ulinzi. baada ya kutua Msimbazi ilimuwia vigumu kupata namba moja kwa moja, nyota yake ikaanza kung’ara chini ya kocha Mkameruni Joseph Omog, akichezeshwa kama mbadala wa Jonas Mkude.

Mechi ambayo Kotei huenda haji kuisahau ni ile ya fainali ya kombe la Azam mwaka 2017, iliyochezewa pale makao makuu, Jamuhuri Dodoma dhidi ya Mbao FC na kuishuhudia Simba ikiibuka na ushindi wa goli 2-1, Shiza Kichuya akifunga goli la penati dakika za lala salama. Katika mchezo huo Kotei ndiye aliyekuwa mchezaji bora “man of the match”, kiukweli aliupiga mwingi hadi aliboa.


Ameitumikia Simba kwa mafanikio makubwa, ameichezea Simba jumla ya mechi rasmi 75 akifunga goli 1 pekee tena dhidi ya Mbao katika sare ya 2-2 kule mkoani Mwanza.

Kwa sasa amesajiliwa na klabu ya Kaizer Chief ya Afrika Kusini kwa kandarasi ya miaka mitatu. Ni ukweli usiopingika kuwa, kuachwa kwa Kotei kumefanya mashabiki wengi wa Simba na wadau wa soka nchini kushindwa kuamini kilichotokea.
Kuachwa kwa kiungo huyu fundi na mkata umeme, kumekuwa kukitafsiriwa katika mitazamo na maono tofauti. Leo nimeona sio mbaya name nikupe sababu 5 za kiufundi za kuachwa kwa fundi huyu James Kotei katika kikosi cha wekundu wa Msimbazi.

1. RIPOTI YA MWALIMU.
Hii naipa hadhi ya kuwa sababu ya kwanza ya kuachwa wa james kotei. Kocha Patrick Aussems alipendekeza kuachwa kwa James Kotei katika repoti yake aliyoiacha kabla ya kwenda mapunzikoni baada ya kuisha kwa Msimu. Umekuwa ni utamaduni uliokomaa kwa kocha kuacha ripoti baada ya Msimu.
Ripoti ya kocha yeyote wa mpira huelezea hali halisi ya klabu, kuanzia kwenye ubora, ubovu na kipi kinahitajika kuongezwa, kocha hupendekeza aina ya wachezaji wanaotakiwa kubaki na wale wanaotakiwa kuondoka.

-Patrick Aussems, kocha wa Simba Sc

Kocha hufanya maamuzi ya kumbakiza au kumuondoa mchezaji kutokana na kiwango cha mchezaji husika katika kipindi husika, mbali na kiwango pia falsafa na mfumo hutumika katika hili.
Msingi mkuu wa hoja hii ni ripoti ya mwalimu. Klabu ya Simba kwa sasa inajinasibu kujiendesha kisasa, ndio maana inahitaji kutii mahitaji ya mwalimu, ili siku wakimfukuza kuwe na sababu ya kufukuzwa kwake.

Jiulize hivi ingekuwa ni kipindi kile cha Ismail Aden Rage ndio mwenyekiti wa Simba unadhani Kotei angeachwa? Tena akiwa katika kiwango kikubwa? Haya yote yanakuja kutokana na ukweli kwamba Simba ya leo inajaribu kujiendesha kisasa kwa kutii ripoti ya mwalimu.

2. MFUMO WA SIMBA
Hoja hii inaelezea hasa, kwanini Kocha Aussems ameamua kumuacha mchezaji kama Kotei. Mfumo ndio kielelezo halisi cha wapi mchezaji anatakiwa kuwepo na kutimiza majukumu gani.
Kocha Patrick Aussems, tangu huko alikotoka kama kocha mkuu, amekuwa akitumia mfumo wa 4-3-3 defensive, yaani viungo watatu wa kati lazima wawili wawe na asili ya kukaba.
Kwa tamaduni na soka la klabu ya Simba, viungo wenye asili ya Simba ni adimu mno kuwapata. Inavyoonekana Aussems ana mpango wa kuleta ladha halisi ya Soka kama burudani ndio maana ameamua kuachana na James Kotei.


JIULIZE KATIKA HILI KOTEI ANA NINI?
Kotei anajua kucheza maeneo mawili pekee, kwanza ni kiungo wa ulinzi, yaani huchezea chini, pili anaweza akacheza kama beki wa kati, bado pia ni kuchezea chini vyote vikimaanisha kulinda.
Kuna wakati James Kotei hucheza kiungo cha chini, kama beki wa kati, \na kujipa majukumu mapya ya ulinzi kinyume na hitaji la mwalimu, Mchezaji kama huyu kitaalamu huitwa Sweeper yaani huigeuza klabu kucheza kutoka mfumo wa 4-4-2 HADI 5-3-2.
Aussems kwa sasa anaonekana kutaka kutumia mfumo wa TOTAL FOOTBALL yenye mchanganyiko na TIKI-TAKA. Mifumo hii miwili haimuhitaji sana Kotei, bali inamuhitaji mchezaji zaidi ya Kotei. Kumbuka kuwa silaha kubwa ya mifumo hii miwili ni matumizi ya Offside trick, kwa kuwa mabeki wao huchezea juu, na kama mabeki huchezea juu maana yake huhitaji kiungo wa ulinzi anayechezea chini muda mote.

3. UBORA WAKE
Kotei ni mbora kwa baadhi ya vitu lakini pia ni mbovu kwa baadhi ya vitu. Ubora wa vitu vyake hauendani na mfumo wa soka la samba chini ya kocha Patrick Aussems.

James kotei ni mzuri akiwa hana mpira kwa maana ni mzuri kuisoma “mikimbio” ya washambuliaji wakati timu ikiwa haina mpira, ni mzuri kukaba kwa kutokea nyuma (blind side defending), na kuingilia mchezo yaani kufanya “Interception”.

Licha ya haya yote, Kotei sio mzuri akiwa na mpira.
Tukumbuke Kotei wa Joseph Omog alimuweka benchi Mkude kutokana na uwezo wake wa kupiga mipira mirefu katika pembe zote za uwanja. Chini ya Aussems, Kotei hakutakiwa kufanya hivyo badala yake alitakiwa kuwa na uwezo wa kukaa na mpira, kuwa na kasi na kutoa pasi fupi kwa usahihi, tena hata kukiwa na utitiri wa wachezaji.

Kotei ameonekana kushindwa kufanya haya. Katika mfumo wa Simba wa kumili mpira, mashambulizi kutokea nyuma, kwenda katikati hadi kwa washambuliaji, Kotei anajikuta hafiti mbele ya Mkude chini ya Aussems.

4. MAWASILIANO MABOVU
Kwa mujibu wa James Kotei, Mwenyewe anadai kuwa, aliipa nafasi kubwa klabu ya Simba kumbakiza baada ya misimu mingi na mizuri aliyoitumikia Simba. Alijua Simba ingemuongeza mkataba. Licha ya kuipa taarifa klabu hiyo kuwa kuna vilabu vingi vinamtaka vikiwemo vilabu vya Afrika ya kusini na nchini Ghana, lakini klabu ilionekana kupotezea vito wake.


Inavyoonekana hakukuwa na mawasiliano mazuri kati ya wakala wa Kotei, Bwana Musleh na klabu ya Simba. Hakukuwa na mawasiliano mazuri kwa maana haikuwa inafaa kwa Kotei kupewa mkataba dakika za mwishoni baada ya mashabiki wa Msimbazi kulalama juu ya kiungo huyo.
Mawasiliano mabovu kati ya mchezaji na klabu juu ya hatima yake na mkataba mpya ni dalili kuwa, kuachwa kwa Kotei kulikuwa ni agizo la kimaandishi kutoka kwa kocha ndio maana hata kamati ya Utendaji ya kalbu ya Simba ilimpotezea Kotei.

5. UWEPO WA JONAS MKUDE.
“The Stoper” nitaachaje kumtaja wakati ndiye mchezaji wenye stamina zaidi ya Kotei, pasi zake nyingi ni sahihi, ni fundi kwa pasi fupi fupi na ndefu.
Ana uwezo wa kupiga mashuti nje ya 18 na bado akafunga, miguu yake ina nguvu nyingi, akiwa na mpira kumpokonya ni vigumu kwa kuwa hutumia miguu yake kuulinda, ni mzuri kupokonya mipira kwa mpinzani.

Ukiniambia nikutajie wachezaji wawili wanaoaminiwa zaidi na Kocha Aussems kwa Simba kwa Sasa, siwezi nikaacha kumtaja Jonas Mkude na John Raphael Bocco.
Mkude na Kotei waote walimaliza mikataba yao, lakini Mkude ameongezewa lakini Kotei akaachwa, SWali je ni kwanini Aussems hakupenda Mkude na Kotei kucheza Pacha?

Inaonekana Aussems anaamini kuwa, kama Mkude atacheza chini ya Usajili Mpya SHARIFU SHIBOUB itakuwa na faida kuipeleka timu mbele kuliko Mkude Mkude kucheza pacha na Kotei.

Faida ya Mkude ni Box To Box Mid fielder yaani anaweza kucheza chini na kupandisha timu, kwahiyo Mkude anaweza cheza kama Kiungo wa Ulinzi, kiungo wa kati na kiungo Mshambuliaji wakati kotei anaweza kucheza kama kiungo wa Ulinzi na beki wa kati.

Kumuacha Kotei ni malengo ya Aussems kufika mbali kimataifa, ukiangalia udhaifu mkubwa Simba katika mashindano ya kimataifa ni kushindwa kufika kwa kasi eneo la mpinzani, hii ilitokana na kuwa na viungo wawili wenye asili ya ulinzi katika eneo moja.

Kwa Mkude atacheza kama kiungo wa ulinzi huku akipanda hadi katikati, huku Shiboub anaweza kuungana na Clatus Chama kushambulia kwa kasi!
Cahnagamoto kubwa inaweza kujitokeza endapo kama, viungo hawa watatu yaani Mkude, Chama na Shiboub watashindwa kuwa na muunganiko. Na hapo ndipo viungo wengine kama Francis Kahata, Hassani Dilunga na Ndemla watachukua nafasi zao kiulaini.

Tafadhali tumia viungo vya mitandao ya jamii kusambaza.