Blog

‘Scout’ ya bure kwa Yanga, fanyeni haraka sokoni.

Sambaza....

Msimu upo Ukingoni, Yanga Ana asilimia 99 za kuwa Bingwa ikiwa ni majibu tosha kuwa, msimu Ujao atakuwa ni miongoni mwa Timu 4 zitakazoiwakilisha Nchi Kimataifa.

Ukitazama takwimu za Yanga ndani ya Ligi Utabaini kuwa ndio Timu inayoongoza kwa kila kitu kizuri.

Hadi sasa ndio timu ilishinda mechi nyingi Zaidi -19. Ndio timu ilifunga goli Nyingi Zaidi 42, ndio timu yenye “ cleansheets” nyingi Zaidi 19. Ndio timu iliyofungwa magoli machache Zaidi 7. Ndio timu haijapoteza hata mechi moja “ Unbeaten” Ndio timu inayoongoza kwa Kucheza Mpira Mzuri Zaidi kwa Kupiga pasi nyingi Zaidi 9891.

Wachezaji wa Yanga wakiwa mazoezini.

Ndio timu inaoongoza kwa kupiga mashuti mengi langoni kwa Mpinzani 308, usije ukasahau Yanga ndio timu yenye Top scorer hadi Sasa, Mayele mwenye goli 14 kwa kufungana na George Mpole wa Geita Gold, lakini pia ina Djuma Shabani anayeongoza kwa pasi za Mwisho 5 akifungana na Abdulahman Musa wa Ruvu Shooting, bila kumsahau Reliant Lusajo wa Namungo.

Hizo zote zilikuwa ni takwimu za ndani ya Ligi; Wadau wengi hujiuliza je Kimataifa Itakuwa ya Moto kama ilivyo katika ligi ya ndani? Jibu la haraka haraka Ni HAPANA. Hapana kwa sababu licha ya Takwimu za Yanga kunona, lakini bado kikosi cha Nabi kina mapungufu mengi tena takribani kwa Kila eneo la kiuchezaji.

Utafiti wa KandandaTz tangu kuanza kwa Ligi na michuano yote Yanga imeshiriki imebaini kuwa, Yanga ina mapungufu katika eneo la Ulinzi, La Kiungo na Ushambuliaji, madhaifu ambayo ili kuyaziba kunatakiwa kuwepo kwa maingizo mapya ndani ya Klabu.

Maingizo hayo sharti yawe ni ya kuisaidia Timu katika michuano ya ndani na ya nje ya Nchi. Kiufupi Yanga wanatakiwa kufanya Usajili wa Maana kuelekea katika michuano ya kimataifa na Msimu Mpya wa Ligi ambapo Kutokana na Ugumu wa Ligi Msimu huu Kandanda tunaamini kuwa Msimu ujao utakuwa Mgumu Zaidi.

Hivyo maandalizi ya Timu hasa kwenye Usajili lazima Kuzingatia na hilo pia. Kandanda tumefanya Utafiti wetu na leo tunakuletea “ Scout Report” kwa Klabu ya Yanga; Hapa tutakuletea wachezaji 7 wanaofiti kusajiliwa na Yanga, ambao kwa Sifa zao na falsafa ya Klabu na Mbinu za Nasredine Mohamed Nabi watafiti na watakuwa msaada kwa Timu katika Ligi za ndani na Kimataifa.

YouTube player

Kumbuka lengo letu ni kuhakikisha timu zetu zinafika mbali Zaidi kimataifa, kwanza ili Kuendelea kushikiria nafasi ya Nchi kuingiza timu nne lakini pia kuleta heshima la Kisoka kwa mataifa mengine, kitu ambacho kinaweza Chochea makampuni mengi kuja kuwekeza katika ligi yetu na hata kubadilisha kabisa taswira ya Biashara ya Soka nchini.

Ambatana na jopo la waandishi wa KandandaTz hadi mwisho wakiipa Yanga nondo.

1. Nickson Kibabage

Huyu ni miongoni wa Wachezaji wanaofanya Vizuri katika Ligi kuu Tanzania Bara kakini pia kimataifa akiwa na timu ya Taifa. Kibabage ni Beki wa Kushoto wa kisasa kabisa mwenye Uwezo Mzuri wa kupanda na Kushuka.

Akipanda hupenda kufika mwisho wa Uwanja na Kipiga Krosi au kupiga pasi ya Ndani. Uzuri wa Kibabage ni mzuri pia kwenye Mipira ya Hamsini kwa Hamsini Ardhini, bila kusahau uwezo wa kumpita adui kwa Kumlamba chenga au kupiga pasi moja ya Ndani kisha kujitenga tena ili kupokea pasi.

Kwa aina hii ya Uchezaji NA ukizingatia Udhaifu ndani ya kikosi cha Yanga katika nafsi ya Beki wa Kushoto ni Kubwa Ukilinganisha na Kulia. Kama kumbukumbu zako zitakuwa sawa utakumbuka kuwa tangu aondoke Gadiel Michael, Yanga imejaribu kuwaleta mabeki wengi wa Kushoto Bila mafanikio.

Unamkumbuka Muharami Issa Marcelo? Jafary Mohamedi, Ally Mtoni (Mwenyezimungu Amrehemu), Adeum Salehe wote walifeli, huku waliopo kwa sasa kama David Bryson na Yassin Mustafa wote wanasumbuliwa na Majeraha, kitu ambacho Humlazimisha Kocha Nabi Kumtumia Kibwana Shomari ambaye kiasili ni Beki wa kulia na farid Musa ambaye kiasili ni kiungo wa kati, Ushambuliaji na winga. Ili kuleta Msawazo wa Kikosi, Yanga inatakiwa kumsajili KIbabage ili Kibwana aende Kuliimarisha eneo la beki wa kulia kwa kuungana na Djuma Shabani.

Hii ndio Njia pekee ya kuziba mapungufu mengi na Uhitaji katika Safu ya Ulinzi kwa mabeki wa pembeni kulia na kushoto pale Yanga.

2. Kialonda Gaspar

Kutoka nchini Angola huyu ni beki wa kati kwa Upande wa Kushoto anayekipiga pale Sagrada Esperance ya Angola.

Umri wake ni Miaka 24, umri ambao kama ni mchezaji basi anaweza kutoa kila alichonacho kwa ajili ya timu lakini Pia shauku ya kufanikiwa kwake ni Kubwa Zaidi. Kimuonekanp Kialonda ni Mrefu, mwenye uwezo mkubwa wa Kupiga pasi sahihi ndefu na Fupi, anajiamini, ni Mtaalamu wa kuokoa mipira ya hewani na Ardhini ile ya hamsini kwa Hamsini.

YouTube player

Kialonda ni fundi wa kuingilia mchezo lakini kubwa kushinda yote ni Utulivu akiwa katika eneo lake, anajituma, sio beki wa mambo mengi. Bila shaka wote tunamjua Henock Inonga Baka wa Simba, Kialonda ni Karba hiyo isipokuwa yeye hana mbwembwe nyingi, yupo “serious” hachekicheki Hovyo wala kutafuta Sifa; anachojari ni kutimiza majukumu yake Uwanjani. Yanga inamuhitaji sana aina ya beki kama huyu, Kwanza ni kutokana na kukosekana kwa Mbadala wa Bakari Nondo Mwamnyeto upande wa kushoto kitu ambacho humlazimisha Kocha Kumtumia Yanick Bangala pindi anapotaka Kumpumzisha Nondo, lakini pili Urefu wake ni msaada sana kwa Yanga ukizingatia uwepo wa Mchezaji kama Dickson Job, Yassin Mustafa na Djuma Shabani ambao wote ni wafupi hivyo kushindwa kuwa wazuri wa Kusafisha MIpira ya hatari hasa ya Angani. Ujio wake Utasaidia “Squad Rotation” lakini pia kuiimarisha safu ya Ulinzi na kuwa ngumu Zaidi.

3. Frank Magingi

Kwa pale Namungo Magingi ni Miongoni mwa mabeki Tough wanaocheza kama beki wa kati hasa kwa Upande wa kulia. Ukitaka kuunda Ukuta Mgumu Zaidi Barani Afrika ni lazima Uwe na Wachezaji Tough na wenye uwezo wa kujituma kwa asilimia Mia moja kama Ilivyo kwa Frank Magingi.





Magingi ni Mzuri wa Kufanya Clearance, Kuingia mchezo, kupiga pasi ndefu na Fupi, lakini pia ana jicho la karibu kwa beki wake wa pembeni na kumsaidia Uokozi pindi anapopitwa.

Ninachompendea Magingi ni Beki Mfia timu, yuko tayari kutoa kila alichonacho ili kuinusuru Timu, huyu ni beki wa Jihad. Kimataifa unahitaji Wachezaji wenye Uwezo wa kujimotivate wenyewe na Nguvu ya kupambana kutoka ndani kama ilivyo kwa Magingi. Magingi hatakiwi kusajiliwa kwa bahati mbaya; Kutokana na Ugumu wa Michuano ya kimataifa, lakini pia Wote tunajua kuwa Ligi yetu nayo imeanza kuwa ya Kibabe, hivyo tarajia Msimu Ujao Ligi itakuwa ngumu mara mbili ya msimu huu, hivyo Klabu kama Yanga ili iweze kutetea Ubingwa wake Vizuri ni lazima iwe na Wachezaji wengi na Wazuri katika safu ya Ulinzi na maeneo mengine.

Yanga inamuhitaji Zaidi Magingi kutokana pia na Nishati aliyonayo; Magingi wa kutumika hata kila baada ya Siku Mbili, anamudu kufanya hivyo, lakini pia Ataufanya Ukuta wa Yanga kuwa Chuma, kwa maana wanaoanza ni Balaa na waliopo Benchi nao Ni balaa.

Pale Namungo bila shaka anapatikana kirahisi Ukizingatia Mwishoni mwa Msimu huu anamaliza mkataba wake; hivyo Yanga ianze kurusha Ndoano mapema. Ikimnasa tu, basi imelamba dume.

4. Victorean Adebayor

Miongoni mwa Wachezaji wapambanaji zaidi ndani ya Niger kama nchi ni huyu Victorien Adebayor, lakini pia ndiye mchezaji hatari zaidi ndani ya klabu ya US Gendarmarie bila kusahau katika ligi ya Niger na timu ya taifa. Pale USGM, Adebayor sio Mshambuliaji usema labla muda wote yupo kwenye Box hapana, Jamaa ni Winga wa kulia, winga teleza, anajua kunyumbulika, Guu lake la Kushoto limejaa Midhahabu na Mialmasi ya kutosha.

Kimuonekano anaonekana kuchoka choka lakini Mpe namba ndipo utakapojua kuwa, Adebayo ni Mtu na Nusu.

Katika mfumo wa 4-3-3, Adebayor huanza pembeni kabisa na Juu kama Wing Foward mara zote akifanya mikimbio yake kutoka pembeni kuingia ndani. Huyu akiwa pembeni anajua vyote, kupiga Krosi na hata kuingia Mwenyewe ndani. Lakini pia katika mfumo wa 4-2-3-1, Adebayo hutumika kama Winga wa Kulia. Umaarufu wa Adebayo hubebwa na Vitu vikuu viwili; kwanza ni Uwezo wake Binafsi alionao wa kukokota mpira kwa kasi, kupiga vyenga, kushuti na kujiweka katika maeneo nyeti kwa kufanya mikimbio sahihi akiwa hana Mpira. Kumpata huyu maana yake Una winga anayejua kufunga, Winga karba ya Msuva, lakini pia Uzoefu alionao Adebayor Utakuwa ni Msaada Mkubwa kwa Klabu kama Yanga ambayo ina misimu mIngi haijashiriki wka Mafanikio Michuano ya kimataifa.

Kikubwa cha ziada ni kwamba, Falsafa Mama ya Yanga ni kuhambulia kupitia pembeni, hivyo kumpata Fundi wa kutumia maeneo ya pembeni maana yake umepata Mchezaji sahihi kwa ligi ya ndani na Kimataifa.

5. Stephen Aziz

Ki Takwimu zinaonyesha kuwa Ukiichukua ASEC Mimosas yote katika michuano ya Shirikisho Afrika; huyu ndiye Mchezaji hatari zaidi katika timu akifuatiwa na Mshambuliaji Kinda Karim KONATE KWA JINA LA KIMAANGAMIZI Wanamuita KOKA.

Uhatari wa Aziz Ki, Upo kwenye vitu kadhaa muhimu, cha kwanza Kasi, pili Uwezo wa Kukaa na mali mguuni, kufunga bila kusahau kucheza maeneo tofauti tofauti. Aziz Ki amekuwa akitumika katika nafasi mbalimbali kulingana na uhitaji wa mechi husika. Kwa Mfano dhidi ya Simba, Asec waliingia na Mfumo wa 4-4-1-1, hapa Aziz Ki alicheza kama Mshambuliaji wa Pili akitokea hasa Upande wa Kulia alikokuwa Tshabalala. Lakini Pia katika Mfumo wa 4-3-3, Aziz Ki huanza pembeni na Juu upande wa kulia kama Wing Forward akifanya mikimbio yake ya kasi kutoka Pembeni kuingia ndani. Vivyo hivyo katika mfumo wa 4-2-31, Aziz Ki amekuwa akitumika kama Winga wa kulia anayeingia ndani na Kutoka.

Kwa staili anayocheza,Aziz Ki ni Kama Francis Kahata aliyechangamka; Kwa maana Ki ana Kasi ya kwenda Mbele, Ki ana piga mashuti Mwana Ukome, Ki anajua Ku- drible Umbali Mrefu lakini pia kupita kwenye Utitiri akitafuta nafasi ya kushuti, Ki anajua kukaa katika maeneo muhimu ya Kupokea na Kutoa pasi. Ki ni hatari zaidi akitokea kulia yaani kwa beki wa Kushoto wa timu Pinzani. Kutokea kulia mara zote humpa Nafasi ya kupiga pasi na mashuti upinde, lakini pia ku-drible na kujipa nafsi nzuri ya Kushuti.

Kucheza kulia ni Bora zaidi kwake kutokana na Mguu wake anaotumia (Mguu wa Kushoto), kwani Aziz Ki sio Mwepesi wa kupiga Krosi, Huchagua kuingia mwenyewe ndani kuliko Kupiga Krosi. Aziz Ki sio Mtamu tu kwenye kushambulia lakini pia kwenye majukumu ya kIulinzi, kwani mara nyingi anaonekana kushuka chini japo kulifikia eneo la kiungo wa Ulinzi. Kwa Mfano katika mchezo dhidi ya Simba nyumbani , Ki alifanikiwa kupiga tackles 2 kwa mafanikio, bila kusahau pasi 27 sahihi, na hata kumfanya kuwa mchezaji aliyefanya vizuri zaidi katika mchezo ule ukimjumuisha na Aishi Manula wa Simba. Kwa Yanga kama Usajili huu Utafanikiwa basi ndio Utakuwa Usajili Bora zaidi kwa Msimu huu huo na Miwili iliyopita. Huyu akija hana haja ya kusubiri Benchi, ataingia moja kwa moja kwenye Kikosi na kuisadia timu.

6. Aubin Kouame

Aubin ni miongoni mwa Vipaji Vichache kutoka Asec Mimosas ambaye ameonyesha Uwezo mkubwa akiwa na Mpira na hata Bila Mpira. Huyu ni miongoni mwa Mawinga wenye Acceleration kubwa, ni mgumu sio laini laini, ni Mzuri akishambulia Pembeni Zaidi, ana kasi, anajua kupiga Krosi, lakini kilicho bora Zaidi Aubin anajua kucheka na Nyavu, yaani anapenda kushuti golini akipata nafasi.

Kwa sifa alizonazo bila shaka wala Wasiwasi; Mawinga kama Jesus Muloko watakuwa hawana namba tena, Mawinga ambao hawawezi kumpita adui wanapokutana One against One; Aubin ni Balaa Jingine, Mawinga ambao hawana maamuzi ya wapi kwa kushuti na Wapi kwa kutoa pasi, Aubin atawakosoa sana. Sifa zote za Winga wa karba ya Raheem Sterling, Mahrez Riyard anazo Aubin, Yanga ikimnasa Aubin itakuwa imejiimarisha katika eneo la Pembeni mwa Uwanja.

Ni Uhakika Yanga itakuwa Ya Moto kila eneo la Uwanja. Kunasa huduma yake ni Rahisi Mno ukizingatia, Asec Mimosas ni kama Academy; ni kiwanda cha wachezaji; wapo pale kwa ajili ya Biashara hiyo, Yanga wakienda watampata siku hiyo hiyo.

7. George Mpole

Hadi sasa takwimu zinaonyesha kuwa Geita Gold chini ya Kocha Fred Felix Minziro Baba isaya imeshinda Jumla ya mechi 9, sare 9 na kufungwa 8 lakini pia imefunga jumla ya magoli 26 pekee. Kati ya goli hizo, Mpole amefunga goli 14 na kutoa pasi za mwisho, hii ni sawa na kusema Mpole amehusika katika magoli 17; Kimahesabu hii ni sawa na Kuhusika katika 64% ya magoli yote.

Wengine kumuona kama Mshambuliaji mwenye Bahati lakini kuna kitu cha Ziada anacho hasa shauku ya Kupiga golini, huhakikisha muda wote anatafuta mazingira na Mpenyo wa Kushuti; Hii ni sifa ya kwanza kwa Mshambuliaji ambapo Mpole anayo. Mpole anaelekezeka na ndio maana kwake kucheza Kimuunganiko na Ayoub Liyanga ambaye humzunguuka na wote kusomana, Mpole akiwa pale juu kama Standing striker Lyanga afanyeje na Lyanda akiwa pembeni mwa Uwanja, Mpole anatakiwa kufanya nini.

Maelewano haya huifanya Geita Gold kuwa hatari kwa klabu nyingi lakini pia mbinu za Baba ISAYA kuonekana kufanya kazi Vyema. Kwa Nyongeza! Mpole ni Mshambuliaji aliye Tough sio laini laini, Inaonekana ana nidhamu kubwa sana wakati wa mazoezi Binafsi na ya Timu ndio maana Vita ya Kugombania Mipira ardhini na hewani huwa sio ishu kubwa kwake lazima ashinde lakini pia Muda mwingi yupo fiti hasumbuliwi na Injuries za mara kwa mara.

Ukizingatia Ligi kwa Msimu Ujao itakuwa ngumu Zaidi, lakini pia Ukitazama na Michuano ya Kimataifa Utaona ni Jinsi gani Yanga inahitaji Mchezaji Karba ya Mpole.

Hadi kufikia hapa Utabaini KandandaTz tunaamini kuwa, Yanga ijayo ni Yanga iliyokamilika katika eneo la Ulinzi, Kiungo wa Kati na Ushambuliaji na Winga kulia na Kushoto.

Magoli mengi ya yanga ya msimu ujao yatatoka kwa Viungo wa Kati na Ushambuliaji yaani pale anapocheza Feisal Salumu Abdallah Feitoto, lakini pia kwa Winga ya pembeni kulia na Kushoto.

Sambaza....