Ligi Kuu

Simba imechelewa kumfukuza Omog

Sambaza....

Ilianza kama tetesi. Ikaja kama uvumi. Hatimaye imekuja kuwa kweli. Simba imeachana na kocha wao Mcameroon Joseph Omog. Kila zuri na baya la Omog litabaki kwenye vitabu vyetu vya kumbukumbu.

Binafsi naamini kuna kosa Simba imelifanya juu ya Omog. Kosa lenyewe ni kuchelewa kumfukuza. Nitakuelezea huko chini jinsi ilivyochelewa na kusababisha madhara.

Omog alishafukuzwa Simba miezi mitano iliyopita. Lakini bado alikuwa na watu wa Simba katika maisha yake ya kila siku. Taarifa za kuondolewa kwake zilianza kutoka kabla ya Mayanja kuondoka. Hapa Simba ilikuwa ikiishi na nyoka ndani kwao, papo hapo wakiwa na madebe ya unga wa sembe. Nini kitatokea au kufuata?

Mchuzi wa mbwa unanywiwa ukiwa wa moto, ukipoa haunyweki tena. Vipi Simba hawakumfukuza Omog wakati ule wanakuja kumfukuza sasa walipotolewa kwenye michuano ya FA na timu ya rafiki yangu Azish Kondo? Hapa Simba wanatakiwa kujilaumu wenyewe kwanza kabla ya kumlaumu Omog.

Siku ya kwanza waliyofikiria Omog hawafai klabuni ndiyo siku hiyo hiyo walipaswa kupeana nae mkono wa kwaheri. Lakini kujifikiria mara nyingi zaidi ndiyo kumewafanya waje kumfukuza muda ambao hawapo tena katika michuano ya FA.

Omog alipaswa kuondoka wakati ule ambao Mayanja aliondoka. Uliona wapi kocha msaidizi anaondoka kocha mkuu anabaki? Hapa Simba walituletea siasa na mwisho wa siasa zao ni kwenye mbinu za Azish Kondo aliyewaonyesha Simba cha kufanya kwa Omog.

Ndani ya timu Omog alishachokwa. Kuna viongozi hawakuwa tena na imani nae. Alishapoteza mvuto kwa mashabiki. Mtu huyu anadumu vipi klabuni kwa siku nyingi kama anaishi mazingira ya namna hii? Simba walipaswa kuachana nae muda mrefu kabla hajatokea Azish Kondo na vijana wake kuharibu hali ya hewa Mtaa wa Msimbazi.

Ina maana Simba walisubiri kutolewa FA ndiyo waamini kama Omog hakuwa akiwafaa? Haya ni mapungufu ya viongozi wetu ambao hawana maamuzi sahihi katika kile wanachokiamini.

Kaka yangu Hajji Manara anavutia kumsikiliza akiizungumzia Simba. Anavutia sana. Mwezi mmoja uliopita alitokeza kumkingia kifua Omog na kupiga mikwara mizito, masikini Manara ile mikwara na sifa zote za Omog imeishia kwenye mbinu za Azish Kondo na hatimaye Omog yuko kwao Cameroon hivi sasa. Maisha hayaendi bila unafiki.

Nani anayejua kama Simba wasingekuwa na Omog wangewafunga Green Warrios? Nani anayejua? Hakuna! Lakini uzito wa kufikiri na kuja na majibu ya ufikiri umeifanya Simba iwe hivi ilivyo, Green Warrios wakisonga mbele.

Unaikumbuka ile BRN? Hapa unamaanisha Big Result Now. Simba waliihitaji mfumo wa BRN kupeana mkono wa kwaheri na Omog, lakini kusigana sigana kwenye maamuzi ya aondoke au asiondoke imeifanya michuano ya FA msimu huu kukosa radha. Kunapokuwa na Simba, lazima Yanga wawepo, kunapokuwa na Yanga, lazima Simba wawepo. Unadhani FA ya msimu huu ina msisimko?

Dakika chache baada ya kipyenga cha mwisho cha mwamuzi Israel Mujuni Nkongo pale Chamazi akimaanisha mpira umeisha na Simba kutolewa, nilikutana kwenye korido za uwanja huo na mmoja vigogo wa TFF akilaani Simba kutolewa. Kigogo huyu hajamaanisha wao kukosa pesa ambazo watazikosa baada ya Simba kutoka, alimaanisha soka kiujumla.

Sijawahi kuwa kocha na sitawahi. Sijui nini kije kunitokea na kunivutia nianze kozi za ukocha. Hivi Omog alikuwa sahihi katika mchezo ule wa Green Warrios kuanzisha viungo watano na kuweka mshambuliaji mmoja?

Ina maana Omog aliwahofia Warrios na kuamua kuwawekea watu wengi kati na mbele kumuacha Bocco peke yake? Anyway nenda Omog, wasalimie Cameroon, msalimie na Et’oo.

Sambaza....
Subscribe
Notify of

0 Maoni
Inline Feedbacks
Tazama Maoni Yote
0
Tungependa kupata maoni yako, tafadhali tuambiax
()
x