Sambaza....

Msemaji wa mabingwa watetezi wa ligi kuu Tanzania bara Haji Manara amesema kuwa licha ya Simba kupoteza mchezo wake wa fainali dhidi ya Waoka mikate Azam Fc katika  kombe la Mapinduzi, wikiendi ya Simba sio mbaya hata kidogo.

“Simba ilicheza juzi (jumamosi) dhidi ya Mwarabu na tukamfanya vibaya, jana Mwanahamis Omari kawa mwanadamu wa kwanza kufunga magoli manne katika dabi ya Simba na Yanga kwa upande wa kina dada, kwetu sisi bado ni raha tu ” alisema Manara.

Manara alitumia fursa hiyo kuwashukuru wachezaji, makocha na wote walioisaidia timu kufika hatua ya fainali katika michuano hiyo na kuwapongeza Azam Fc kwa kusema kuwa, Azam walistahili kuubeba ubingwa huo.

Katika mchezo huo wa Mapinduzi uliochezezwa kule visiwani Zanzibar, Azam Fc waliibuka na Ushindi wa goli 2-1 huku wakionekana kutawala takribani sehemu kubwa ya mchezo. Magoli ya Azam yalitiwa kimyani na Mudathir Yahaya na Obrey Chirwa na kwa upande wa Simba Sc, Yusuph Mlipili ndiye aliyekuwa mtetezi wao.

Licha ya Azam Fc, kushinda taji hilo la tatu mfululizo na kupata zawadi ya pesa tashlimu Shilingi milioni 15 za kitanzania, wadau wengi wa soka nchini  wanaiona Azam kama timu ambayo bado haina makali ya kutisha timu zingine zinazoshiriki ligi kuu kutokana na aina ya uchezaji wake.

Licha ya kuingiza kikosi chake cha kwanza katika mchezo huo dhidi ya Simba, Azam walionekana kuzidiwa katika baadhi ya vipindi hasa eneo la kati lililokuwa likimilikiwa na  Haruna Niyinzima na Mohamed Ibrahim. Wadau wengi waliendelea kuizonga Azam na kudai kuwa kama watacheza hjivi bila kuimarika popote wasahau kuchukua ubingwa wa ligi kuu Tanzania bara.

Ukiachana na kombe la mapinduzi, ligi ya wanawake nchini (Serengeti Lite Women’s Premier League) imeendelea jana, huku Yanga Princess ikiwakaribisha Simba Queens katika mchezo wa raundi ya tano, Yanga Princess walikubali kulala kwa jumla ya magoli 7-0 huku Mwanahamisi Omari akiingia katika historia baada ya kufunga goli nne peke yake.

Sambaza....