Zamani

Thierry Henry hakupaswa kushangilia kwenye msiba

Sambaza....

Moja ya vitu vinavyoniumiza ni kuona jinsi wachezaji wanavyoanguka ghafla uwanjani na kufa, ni huzuni!

Ni wachezaji wengi wamekufa uwanjani lakini napokumbuka matukio haya fikra zangu haziachi kunirudisha mwaka 2003 kwenye michuono ya shirikisho ya mabara huko Ufaransa.

Kikosi cha Cameroon kilichoshiriki michuano ya kombe la Mabara mwaka 2003.

Afrika iliwakilishwa na mabingwa wa bara hili 2002 wazee wa mpira kazi Cameroon. Nakumbuka simba hao wasiofugika walikuwa hawana utani uwanjani, walikuwa bora sana. Walikuwa na mastaa wengi kama Eto’o, Patrick Mboma, Geremi Njitap, Patrick Mboma, bila kumsahau fundi Marc Vivien Foe.

Ni tarehe 26 Juni 2003 mechi ya robo fainali kati ya Cameroon na Colombia. Sitosahau nilipomuona Marc Vivien Foe ameanguka, binafsi nilijua ameanguka tu lakini sio amefariki. Baada ya mechi kuisha ndipo nikasikia Foe hayupo tena pamoja nasi, mambo yaliharibika!

Wachezaji wa Cameroon na Colombia wakiwaita madaktari haraka baada ya Marc Vivian Foe kuanguka akiwa pekeake uwanjani.

Pamoja na mkasa huo Cameroon ilitinga fainali kwa ushindi wa goli 1-0.

Kipindi hicho sikuwa mzalendo sana kama sasa, na siku zote huwa ni shabiki damu wa Ufaransa. Hata fainali nilikuwa na chama langu la Ufaransa huku safu ya ushambulizi ikiongozwa na mchezaji wangu bora wa muda wote Thierry Henry, hunambii kitu kwa huyu mwamba.

Nakumbuka mechi hiyo jinsi manahodha Rigobert Song na Marcel Desailly walivyoingia uwanjani wamebeba picha kubwa ya marehemu Marc Vivien Foe. Ilikuwa ni huzuni, na furaha ni ya kulazimisha tu.

Manahodha wa Ufaransa na Cameroon Marcelly Desaily na Rigobert Song wakiingia uwanjani katika mchezo wa fainali na picha ya Marc Vivian Foe.

Kama kawaida Cameroon hawakuwa wanyonge pamoja na msiba mzito. Mechi ililazimika kwenda dakika za nyongeza baada ya suluhu ya dakika 90.

Katika dakika ya 97 Thierry Henry alifunga goli la dhahabu lililomaliza mechi hapo hapo. Kitu kilichonishangaza na kujiuliza katika msiba kama ule Thierry anawezaje kushangilia kiasi kile!?

Thiery Henry akifunga bao mbele ya Rigobert Song na kipa wa Cameroon katika mchezo wa fainali.

Hadi leo sijawahi kupata jibu lakini naamini Henry hakupaswa kushangilia kwa kiwango kile.

Sambaza....