Blog

Usiku wa Balaa!

Sambaza....

Kijana mwenzangu wa zamani je unalikumbuka gazeti la *“SANI”*  enzi zake lipo kwenye *“peak”* miaka ile ya zamani tulipokuwa vijana wadogo? Kama unalikumbuka bila shaka utakuwa unaikumbuka hadithi moja ya kusisimua sana kutoka kwenye gazeti hilo ikiitwa *USIKU WA BALAA!*

Basi juzi usiku katika Uwanja wa Mzee Benjamin William Mkapa maarufu kama *“Kwa Mzee wa Lupaso”* kulikuwa na *USIKU WA BALAA!*

Kanoute akipiga mpira katikati ya wachezaji

Kwa nini ninasema kuwa pale Lupaso juzi usiku ulikuwa ni usiku wa balaa?
Ulikuwa usiku wa balaa kwa sababu kama mbili hivi, kwanza presha tuliyokuwa nayo mashabiki wa Simba kuanzia waliokuwa uwanjani na sisi tuliokuwa majumbani na makazini. Hii pia ilikuwa hata kwa wachezaji wetu katika kipindi kile cha kwanza.

We hebu fikiria mechi ingeisha kwa sare ya aina yoyote ile katika usiku ule mkubwa wa manani ingekuwaje?

Sababu ya pili ya kuuita usiku ule kuwa ulikuwa usiku wa balaa ni kwa jinsi timu ya Gendarmerie namna ilivyokutana na kipigo kizito. Hakika ule kwao ulikuwa usiku wa balaa! Maana walipigwa na kitu kizito!

Mashabiki wa Simba Wakishangilia

Kuwakumbusha tu wasomaji wangu kuwa *Simba Sponga* juzi ilikuwa ni mara yake ya pili kukutana na timu hizi sijui ni za majeshi au Mgambo zenye majina hayo yanayosadifu jina hilo nililolitaja la Gendarmerie.

Miaka mitatu nyuma ilikuja timu hapa yenye jina kama hii timu ya jana kutoka *Niamey* nchini *Niger.* Timu hiyo ilitoka katika *Pembe ya Afrika, ( Horn of Africa)* kule nchini *Djibouti.*
Nilikuwepo uwanja mkuu wa Taifa ambao siku hizi ni uwanja Mzee Mkapa na niliyashuhudia magoli ya *Hamisi Said Ndemla, John Raphael* *Boko* na *Emanuel Okwi*  kwenye kile kipigo cha magoli 4-0 ambacho timu hiyo kutoka kule katika Pembe ya Afrika ilikipata. Mechi ya marudiano nchini Djibouti wenyeji hao walilala nyumbani kwao kwa bao 1-0 bao la *Emanuel Okwi.*

Okwi alipokuwa Simba

Mechi ya jana ambayo nimeona niite mechi ya usiku wa balaa ilinikuta nikiwa zamu kazini kwangu lakini bahati niliyokuwa nayo ni muda uliochezwa mechi hii huku katika idara yangu nikiwa na wanafunzi wangu wawili ambao kusema kweli baada ya mafunzo yao kwa vitendo kwa karibia miezi mitatu sasa naweza kusema kuwa kwa kiasi fulani siwezi kuwa na mashaka nao ninapowaachia eneo letu la kazi na ndivyo ilivyokuwa jana katika usiku ule wa balaa niliwakabidhi vijana ofisi, dogo janja *Kassim* na dada *Edna,* nami nilijongea kwenye baa ya nje kwa maana ya baa iliyopo bustanini hapa kazini kwetu na kuangalia pambano lile lililokuwa na presha kubwa.

Mugalu akifunga bao lake

Kassim yeye ni mshabiki wa *upande wa pili* na aliniambia wazi wazi kuwa anko leo lazima mnafungwa magoli 2-0, nami nikamwambia asante nashukuru.

Huwa yasemwa kuwa mpira mtamu kuutazama mkiwa wengi, watoto wa mjini wanasema *“vibe lake linakuwa si la kitoto”*  hasa kama timu yenu inafanya vizuri.
Mimi nilikuwa peke yangu huku nikipewa maneno makali na ya kukatisha tamaa na mfanyakazi mwenzangu muhudumu wa kike aitwaye *Roda* . Yeye ni mshabiki wa upande wa pili pia kama ilivyo kwa Kassim hivyo alikuwa ananiponda balaa hasa baada ya kuwa mpaka mapumziko mchezo ukiwa hakuna timu iliyokuwa imepata bao lolote. Ilipofika muda wa kufunga ofisi Roda aliondoka na kuuacha mchezo huo ukiwa bado 0-0.

Kanoute baada ya kufanya yake

Wakati *Sadio Kanoute* anaitanguliza *Simba Sponga* kwa bao ambalo alikuwa na utulivu mkubwa sana ndani ya box baada ya kupata ile tunaita *“a well calculated pass”* kutoka kwa *“Super Ben,”* kumbuka kuna magoli kama mawili hivi ya wazi *Kanoute* alikosa katika kipindi cha kwanza, basi mzee wenu nilinyanyuka kitini na kuisogelea runinga huku nikipiga makofi ya nguvu, makofi yaliyomsogeza mgeni mmoja wa Kiasia aliyekuwa nje akivuta sigara kuja mahali nilipo. Jamaa akawa ananishangaa tu mzee mzima ninavyochizika. Bao hilo pia lilimtoa lindoni kwake mlinzi wetu na kukimbilia mapokezi kwenda kuangalia marudio. Mlinzi huyo ni mshabiki mkubwa wa upande wa pili. Bila shaka alikuwa anataka aje na maneno ya michongo kuwa magoli hayo ni ya offside 😜😜  Ndo ujue sasa kuwa soka ni zaidi ya ukichaa!
Wakati *“Super Ben”  Bernard Morrison* *“akimwaga tena upendo”*  kwa mara nyingine na *Chris Kope Mugalu* kufunga bao la pili, katika ile *“brace”* aliyoipata juzi, *(mchezaji anayefunga magoli mawili katika mchezo mmoja kitendo hicho kinaitwa “brace”)* nilijikuta tena ninanyanyuka na kupata *“wehu”* wa muda na kushangilia bao la pili kama *“mwendawazimu”!* Mugalu alifunga magoli yale mawili katika mazingira magumu sana, mazingira ambayo alichofanya ni iioe tunaita mchezaji hutakiwi kukata tamaa bali unapambana kuhakikisha mpira unqingia ndani ya nyavu.

Morrison (katikati)akifanya yake

Goli la tatu sikumbuki nililishangiliaje lakini naamini kabisa nilikuwa katika hali ambayo si ya kawaida kwa furaha ya ushindi.

Kila nilipokuwa nashangilia nilikuwa nasikia mtaani karibu kabisa na ofisini kwetu mashabiki wa Sponga nao wakijibu kwa nguvu kutokea huko katika Kibanda umiza!

Goli la nne nililishangilia lakini siyo sana bali kwa mshangao. Nilimsikitikia sana yule bwana mdogo golikipa wa Gendarmerie kwa kosa kama lile la jana lililopelekea yeye kujifunga. Lakini simlaumu yeye hata kidogo bali namlaumu yule mchezaji aliyemrudishia mpira ule wa *“kimo cha mbuzi wa Pasaka”* kwa nguvu hivyo kupelekea ile *“Jabulani “* kumfanyia *“harusi”* na kupita kwa kasi kwenda kujikita kwenye nyavu zile za chini za goli lile la Kusini mwa uwanja wa *“Estadio De Lupaso”!* huku *“Kifaru cha Kinyarwanda kilichotengenezwa Urusi ya Putin”* kikihakikisha kuwa kwa namna yoyote ile yule bwana mdogo hawezi kuuokoa mpira ule ambao kusema kweli kwake yeye kama golikipa ilishakuwa *“Too late, not to catch a train, but to save a sinking boat”!*
Lakini hutokea golikipa kufungwa magoli kama yale. *Unakumbuka Mtani Jembe?* Basi tusimuhukumu sana yule golikipa. Unamkumbuka pia mchezaji wa zamani wa *Liverpool,* *Stanny Collymore?* Aliwahi kufunga goli katika mazingira kama yale ya goli la nne pale alipopiga akitegemea kuwa hakupiga sawasawa hivyo mpira golikipa ataudaka tu. Lakini kwa mshangao akaona mpira umetumbukia nyavuni. Hakushangilia goli hilo bali akabaki anashangaa!

Nguvu Moja

*Simba Sponga* katika usiku ule wa balaa hawakutaka kufunga goli la tano bali waliamua kuuhitimisha mchezo kwa soka la *“Kihispaniola”*  kwa kugongeana pasi miongoni mwao mpaka pale Refa yule *“White”* na mwenye msimamo mkali uwanjani kutoka *Angola* koloni la zamani la *Ureno,* alipopuliza filimbi ya mwisho.

Katika soka wakati mwingine inabidi kuwaheshimu wapinzani wako hasa baada ya kuwa umepata kile ulichokitaka katika soka, kwa maana ya ushindi maridhawa, ushindi wa kuridhisha, ushindi wa kutosha.

*Ike Cassilas* aliyekuwa golikipa na nahodha wa timu ya Taifa ya *Hispania,* kwenye fainali za *Euro 2012* kule nchini Urusi na Ukraine, *(leo nchi hizi zinapigana vita, wazungu nao aisee)*  baada ya timu yake kuifunga *Italia* Magoli 4-0, aliwafuata wachezaji wenzake na kuwaambia kuwa tuipe heshima Italia, magoli haya ni mengi yanatosha si vizuri kuwafunga tena.

Juzi magoli yetu yalikuwa matatu, goli la nne, Gendarmerie walijifunga kwa presha tu ya Simba Sponga.

Mwisho lakini si kwa umuhimu, nilipenda wale mashabiki wa Simba waliochanganyika na *“mashabiki wachache wa Gendarmerie”*  waliosafiri kutoka *“Niamey  nchini Niger”* kuja kuishangilia timu yao.  Pamoja na rangi ya jezi zao na pia kuchanganyika na mashabiki wa Simba kwenye majukwaa lakini hawakupata buguza yoyote ile. Wakishangilia kwa uhuru kabisa, tabasamu nene na bashasha tele huku wakiwa na matumaini ya *Mnyama* yamkute kama yaliyomukuta siku na mechi na *Jwanang Galaxy!* Walitaka *tufe mara mbili?* Tutawaona wao *KAMA WATARUDI NA ROHO ZAO!* Daaaah! Kwa kitendo kile cha kuchanganyika mashabiki wageni na wale wa Simba Sponga ni jambo la kimichezo sana.
What a sportsmanship!
Tunatakiwa tuwe hivyo siku zote maana soka si uadui soka ni urafikihakuna haja ya kumbuguzi mpinzani wako dawa pekee ni kuhakikisha kuwa unapata matokeo ili kuweza kumnyamazisha.

Picha zote kwa hisani ya Simba Sc


*Karibu sana pia kwenye baa yetu iitwayo* *MZEE PAA & BABU DONKO PUB* na mgahawa wetu ujulikanao kama *GARLIC & GINGER RESTAURANT, MAJOHE, BWERA KWA MCHIKA, GONGOLAMBOTO, DAR ES SALAAM. TANZANIA.

Sambaza....