Mabingwa Afrika

Zesco lazima wafe-Aussems

Sambaza....

Kocha Mkuu wa klabu ya Simba, Patrick Aussems amesema ana imani kubwa na kikosi cha Yanga kwamba kinaweza kuwafunga Zesco United na kutinga hatua ya makundi ya michuano ya Klabu Bingwa Afrika.

Kikosi cha Yanga leo kinaelekea jijini Mwanza, kuweka kambi ya siku 10 kwa ajili ya mchezo huo ambao unatarajiwa kupigwa Septemba 14 uwanja wa taifa, Dar es Salaam.

Aussems ameuambia mtandao wa SportPesa News kwamba anatambua kuwa Yanga wana kikosi bora na imara hivyo kama watajipanga vizuri ana uhakika watafuzu kucheza makundi.

“Sina hofu na Yanga natambua wachezaji pamoja na kocha wanajua umuhimu wa kucheza hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa hivyo kitu cha msingi ni kila mmoja ahakikishe anatimiza wajibu wake,” amesema Aussems.

Katika msimu wake wa kwanza nchini Tanzania, Mbelgiji huyo alifanikiwa kuwaongoza Simba kucheza hatua ya robo fainali ya ligi ya mabingwa Afrika kabla ya kuondoshwa na TP Mazembe.

Kwenye michuano ya msimu huu, Simba wameondoshwa kwenye hatua ya awali dhidi ya UD Songo ya Msumbiji kwa goli la ugenini baada ya kutoka sare ya 1-1 jijini Dar es Salaam kufuatia sare ya 0-0 ugenini.


Sambaza....
Tafadhali tumia viungo vya mitandao ya jamii kusambaza.