Blog

Ajib, Sure Boy, Aiyee, kuna vitu hamjaviweka sawa!

Sambaza....

“Kwangu mimi Rakitic ndio mchezaji anayechukuliwa poa zaidi duniani, ni mchezaji mzuri kwa kila daraja, anafanya kazi nzuri ya ulinzi, hasa kwa upande wa kulia mwa Messi,ana kasi, katika umiliki wa mpira yuko vizuri, mwepesi, ni muwajibikaji haswa! Ni miongoni mwa wachezaji wanaochukuliwa poa sana….

“ acha nimalizie hivi, maana hakuna anayemtaja kama mchezaji mwenye jina kubwa, lakini kwangu mimi, Rakitic anahitajika kuboresha Instagram na mitandao  yake ya kijamii, kwasababu katika ulimwengu wa sasa vitu hivi ni muhimu sana…. Na kwa bahati mbaya yeye hayuko vizuri huko, yeye ni uwanjani pekee..”

Hayo ni maneno adhimu ya Jose Mourinho wakati akifanya uchambuzi wa mechi ya Real Madrid dhidi ya Barcelona katika kituo kimoja cha televisheni.

Maneno hayo hayamuhusu Ivan Rakitic pekee bali ni wachezaji wote duniani. Lakini mimi nitawaangazia wa Tanzania pekee kwakuwa wengi nawaona wako karne ya 21 lakini maisha wanayoishi katika soka ni ya karne ya 19.

Kila nikizitembelea kurasa za wachezaji wetu katika mitandao ya kijamii, naziona hazina maudhui, yaani hawaweki kitu chochote cha maana kulinganisha na vile vingi wanavyofanya.

Sijui kama hata wanaelewa faida ya kuweka vitu kwenye mitandao yao ya kijamii !, huenda hawajui mpira ni biashara. Biashara hii ipo katika pande mbili yaani upande wa klabu na kwa mchezaji binafsi. Hapa naangalia hasa kwa mchezaji binafsi.

Unakuta mchezaji hana hata “facebook page” unadhani atawakusanyaje mashabiki wake?.mchezaji mwingine huenda ndio mfungaji bora hata ligi, au yeye ni kiungo matata, akiwepo yeye dimba linatulia, lakini masikini ya Mungu hajui kutumia kipaji chake kujitangaza zaidi kwa lengo la kibiashara.

Biashara tu ndio inayomfanya Cristiano Ronaldo kuwa mchezaji tajiri, ukiachana na fedha anazolipwa kutokana na soka analocheza, Ronaldo anakula shavu kwenye makampuni mbalimbali kutokana na umaarufu wake. Hata hivyo “accounts” zake za mitandao ya kijamii zimenona.

Mwaka 2018, Ronaldo ndiye aliyekuwa binadamu mwenye wafuasi wengi zaidi katika mtandao wa Instagram. Alikuwa na followers 144,482,390. Hivi mchezaji mwenye mashabiki wengi hivi unadhani ni ngumu kupata makampuni hata ya kutangaza bidhaa zake! Tayari huyo ana ushawishi, kwahiyo kila kitu kwake ni rahisi.

Sawa! Tunajua wachezaji mambo mengi, basi kuwa na mtu wa kukufanyia kazi hiyo, japo kuiweka mitandao yako ya kijamii kuwa “active” muda wote. Kupata  mashabiki kwenye mitandao ya kijamii, kunahitaji uwekezaji wa muda na wakati mwingine wa kifedha pia.

Ronaldo alishawahi kuulizwa, angependelea kuwa kocha baada ya kumaliza kipindi chake kama mchezaji? Akajibu hapana, bali angependa kuendeleza biashara zake, alizozianzisha akiwa mwanasoka.

Kila mtu ana mawazo yake baada ya kumaliza karia yake, lakini mwenye mawazo ya kibiashara na kutengeneza pesa huwaza katika muktadha wa Ronaldo. Lakini sharti kwanza lazima uimarishe mitandao ya kijamii, kwani ni rahisi kutumia mitandao hiyo kujiinua kiuchumi kwa kutangaza biashara zako na hata za wengine kikubwa utengeneze pesa.

Haji Manara, ni msemaji tu, lakini amebaini nini kipo ndani yake, nani kivipi anaweza akakitumia kutengeneza pesa. Na amefanikiwa hadi kuwaajiri watu wa kusimamia umaarufu wake. Instagram ana followers laki 9 pekee, tayari anakula shavu kwa kampuni ya maziwa na kampuni ya kubeti, pia ana kampuni yake. Hivi vyote vinamaanisha PESA TU.

Mchezaji ana muda mfupi sana kubaki katika tasnia na kutengeneza pesa. Bila shaka ni miaka hadi 35 tu hivi kwa hapo Tanzania, mchezaji atakuwa ameshastaafu soka. Lakini pia mchezaji anaweza kujitengenezea kesho yake nzuri zaidi baada kumaliza soka kama tu atajiandaa vizuri.

Kujiandaa vizuri ni kutumia wakati uliopo na fursa ya umaarufu inayokuzunguuka kutengeneza pesa kwa maisha ya kesho. Nilifurahi kukutana na tangazo katika ukurasa wa facebook wa JAMES KOTEI wa Simba. Naye kiukweli anajitahidi kuweka vitu, wengine kwa mwezi wanaweka “content” mara moja tu.

Kuna wachezaji hapa Tanzania, hata ukimtafuta kupitia ‘google’ hukutani na taarifa zake. Huu uzembe unaanzia kwa klabu yake, klabu zetu zimekuwa zikiendeshwa kana kwamba hazipo katika dunia hii tunayoishi. Hawaweki hata taarifa za klabu mtandaoni kila mtu azione akizitafuta.

Huwa sijui hivi hawa wanaojiita “communication officers” wasemaji huwa wanafanya nini? Klabu haina hata tovuti, na hata ikiwa nayo bado unakuta haina kitu. Zingine zina habari za mwaka 2017 wakati sasa tupo mwaka 2019. Tovuti ya klabu haina kitu hadi mwezi mzima kana kwamba klabu haina shughuli yoyote ndani ya huo mwezi.

Licha ya hayo yote, mchezaji ana jukumu la kujitangaza kibinafsi kwa faida zake binafsi. Kuna wachezaji wangapi walicheza katika viwango vikubwa tu na kwa sasa maisha yao hayaendi poa? Na wao walicheza kipindi ambacho mitandao ya kijamii haikuwa mikubwa kiasi cha kuwa tengezea pesa. simu zenyewe zilikuwa adimu, hao followers wangepatikana vipi?

Lakini wachezaji wetu wamebahatika kucheza mpira kipindi ambacho dunia imepanuka, kimekuwa ni kijiji kimoja, mifumo ya kuwaunganisha watu imekuwa imara na bora lakini cha kushangaza kwao hiyo sio fursa. Wakati kwa wachezaji wa Ulaya ni fursa kwa Tanzania sio fursa kabisa.

Kuna mchezaji yeye hana hata video ya dakika 5 pekee kuonyesha maajabu yake uwanjani, hakuna! Zana Coulibaly baada ya kusajiliwa Simba, watu wengi walimtafuta kwenye mitandao ya kijamii na kwingineko kujua undani wa uwezo wake, lakini tayari alishaandaa video yake na kuiweka Youtube inayoonyesha vitu vyake.

Haya ya Coulibaly ndio tunayoyataka, hata kama  klabu haina taarifa za wachezaji wake mitandaoni  basi mchezaji aweke taarifa zake binafsi. Na huo ndio utambulisho tosha kwa mchezaji na kujitengezea fursa zaidi ya kujulikana na watu wote duniani.


Sambaza....
Tafadhali tumia viungo vya mitandao ya jamii kusambaza.