Sambaza....

Klabu ya soka ya Lipuli imethibitisha kupokea barua kutoka katika vilabu viwili vikubwa vya Young Africans na Azam FC za kumuhitaji mshambuliaji wao kinda Adam Salamba.

Lipuli ambao hapo jana walikanusha kupokea barua kutoka Yanga, wamethibitisha kupokea barua kutoka katika miamba hiyo ya soka nchini na kuongeza kuwa mbali na Yanga pia Azam wameonesha nia ya kumsajili mshambuliaji huyo wa zamani wa Stand United.

“Yanga wametuletea barua rasmi na wameweka maelezo ya kwanini wanamuhitaji Salamba, lakini haijaishia hapo, pia Azam wameleta barua rasmi ya kumuhitaji mshambuliaji huyo,” amesema Clement Sanga ambaye ni Afisa habari wa klabu ya Lipuli.

 

“Uamuzi tunaouchukua sasa ni kuwaandikia barua kuwajibu kwa sababu wameonesha uungwana kwa kuja kiofisi, hivyo tutawajibu mapema iwezekanavyo na baadae tutaeleza mambo yanakwenda kwa mtindo upi kama kutakuwa na haja ya kmuuza mchezaji huyo basi yote mtafahamu,” Sanga ameongeza.

Ombi la Yanga

Ijumaa kupitia kwa katibu mkuu wa Klabu ya Yanga, Charles Boniface Mkwassa ilithibitika kuwa Yanga waliiandikia barua kumuhitaji mchezaji huyo kwa ajili ya michezo ya Kombe la Shirikisho barani Afrika hatua ya makundi ambayo inaendelea kwa Yanga kupangwa kundi D pamoja na timu za Gor Mahia, USM Alger na Rayon Sports.

Hivyo kuingia kwa Azam katika vita hiyo inamaana kutawafanya Yanga kukumbana na kizingiti kikubwa kuliko matarajio yao ya kumpata kirahisi mchezaji huyo bora wa ligi kuu kwa mwezi Machi.

Sambaza....