Mabingwa Afrika

Simba ina wachezaji wanne pekee wanaofaa katika hatua ya makundi.

Sambaza....

“katika majukumu yangu yajayo kama kocha, sitasaini mkataba hadi pale klabu itakaponiambia malengo yake na nini watafanya kutimiza malengo hayo” Jose Mourinho.

Ni maneno machache sana kimuonekano lakini yana maana kubwa katika soka la dunia ya sasa. Mourinho alichokuwa akimaanisha kuwa,  aina ya malengo ya klabu lazima yaendane na uwekezaji wa klabu kwa malengo hayo.

Mfano,  klabu inataka kuwa bingwa wa Afrika, lazima iwekeze vizuri kwenye mifumo yake ya uendeshjaji na wachezaji wake lazima waendane kiviwango na ugumu wa mashindano yenyewe.

July 19, mwaka jana, mikoba ya kukinoa kikosi cha Wekundu wa Msimbazi ilikabidhiwa rasmi kwa Mbelgiji Patrick Aussems. Aussems alipewa Simba na kukabidhiwa malengo ya timu, ambayo yalikuwa ni mawili, moja ni kuhakikisha Simba inatetea ubingwa wake wa ligi kuu Tanzania bara, pili ni kuivusha Simba katika hatua ya makundi klabu bingwa Afrika.

Kocha wa Simba Sc, Aussems

Kuendana na malengo hayo, klabu ikaamua kuongeza nguvu kwa kusajili baadhi ya wachezaji. Simba ilimsajili Paschal Sergie Wawa, Clatus Chama, Meddie Kagere, Adam Salamba, Hassan Dilunga, Zana Coulibaly, Vitalis Mayanga, na kuwapandisha Rashidi Juma na  Abdul Suleiman kutoka kikosi B. hiyo ndiyo dhana halisi aliyokuwa  nayo Jose Mourinho na hata Simba.

Wachezaji wote walioongezwa wanafaa katika hayo malengo makuu mawili ya klabu, yaani kutetea ubingwa, na hilo linawezekana kwa asilimia zaidi ya 50, japo kutakuwa na ugumu mkubwa kutokana na ugumu wa ligi hasa katika duru la pili.

Lengo la pili, chini ya Aussems nalo tayari limeshafanikiwa, kwani Simba imeshafuzu hatua ya makundi tena kwa kishindo. Ilifuzu baada ya kuifunga Mbabane Swallows nje ndani kwa jumla ya magoli 7-1, kisha ikaitungua Nkana Red Devils ya Zambia kwa jumla ya magoli 4-3. Hadi kufikia hatua hii, kocha Aussems ameshatimiza nusu ya mahitaji ya mkataba wake na malengo ya timu.

Simba ikajikuta ipo kundi D, kukwaana na vigogo Al Ahly, JS Saoura na AS Club Vita ya Congo. Mechi ya kwanza, Taifa dhidi ya Saoura, Simba ilishinda 3-0, Mechi ya pili dhidi ya AS Club Vita Ugenini ikapigwa 5-0, na mechi ya tatu dhidi ya Al Ahly ugenini imepigwa tena 5-0. Kwa anayeyajua malengo ya timu hata hashangai vipigo hivyo.

Kikosi cha Simba dhidi ya AS Club Vita.

Katika mchezo dhidi ya Al Ahly, Simba walizidiwa katika kila idara, yaani mashuti 11 kwa 9 ya Simba, yaliyolenga lango 6 kwa 2, umiliki wa mpira 71% kwa 29% za Simba, pasi 749 kwa 300, usahihi wa pasi 88% kwa 74% za Simba, faulo 10 kwa 16 walizofanya Simba, kadi za njano 0 kwa 1 ya Simba kwa takwimu hizi utajua nini namaanisha nikikwambia Simba inacheza hatua hii lakini sio sehemu ya malengo yake.

Mashabiki wa Al Ahly katika mchezo dhidi ya Simba.

Hadi sasa, msimamo katika kundi D, unaonyesha kuwa Al Ahly wako kileleni kwa alama 7, wakifuatiwa na Vita Club wenye alama 4, Simba katika nafasi ya tatu na alama zake 3 na JS Saoura akibuluza mkia na pointi zake 2. Hadi sasa Simba ndio timu inayoongoza kwa tofauti kubwa ya magoli ya kufunga na kufungwa, imefunga goli 3 na kufungwa goli 10 tofauti ya -7, Saoura wanafuatia wakiwa na tofauti ya goli -3, vita wana faida ya goli 3 mkononi na vinara Al Ahly wana mtaji wa goli 7.

Katika mashindano haya, tena kwa hatua ya makundi, wachezaji wa Simba wanaofaa kwa ajili ya hatua hii nawaona wako wanne tu, wengine wote wanafaa kutetea ubingwa wa ligi kuu na kuifikisha timu hatua ya makundi lakini mechi za makundi zina wachezaji wake. Ukiambiwa Simba ina wachezaji wa kawaida ni pale inapokutana na timu kubwa, ndio utaamini hiki ninachokwambia.

 Wachezaji hawa wanne ndio nawaona wana uwezo wa kucheza dhidi ya timu kubwa yoyote Afrika na bado wasizidiwe na presha ya mechi na  bado wakaweza kuhimili mikikimikiki ya timu pinzani na hata kubeba ubingwa wa Klabu bingwa Afrika.

Nayakumbuka sana maneno ya Mchezaji bora wa dunia mara tano, Cristiano Ronaldo kuhusu soka na siri ya kuwa kipanga wa kimataifa.

“kipaji ni muhimu, lakini sio kitu cha msingi katika soka”  Ronaldo.

Kuthibitisha maneno yake, jaribu kujiuliza ni wachezaji wangapi wanatamba wakiwa na miaka 16, lakini baada ya hapo wanapotea kabisa katika ramani ya soka? Ni kweli wana vipaji lakini je wanafanya nini ili kujiweka juu muda wote? Kuna kitu cha msingi kabisa kwa mchezaji wa soka ukiachana na kipaji, nah ii ndio inayonifanya nikwambie kuwa, pale Msimbazi kuna wachezaji wanne tu wanao-fit hatua ya makundi klabu bingwa Afrika.

Wachezaji wanne ndio wana vipaji lakini wana kitu cha ziada wakiwa uwanjani, kwanza wanajiamini, wapambanaji na wanaufurahia mpira, yaani ndio kazi yao. Kuna wachezaji wengi bado hawajitambui, hawajui  kusakata kabumbu kunahitaji nidhamu na kujituma kama zilivyo kazi zingine.

Huenda hawajui hilo, na wanahitaji kuwezeshwa kifikra, lakini ukimuuliza leo kocha msaidizi wa AS Club Vita Lau Shungu, kuwa wanawasaidiaje wachezaji wao kulitambua hili atakwambia hivi;

 “Tunafanya mazoezi ya nguvu sana, tunawaweka sawa wachezaji kisaikolojia waamini kuwa maisha yao ni soka”

Saikolojia ya wachezaji lazima iwathamini wao wenyewe na kujiona bado wanahitaji kufanikiwa zaidi katika kipindi chao cha usakataji kandanda.

Simba kwa sasa ina wachezaji zaidi ya 25, wote hawa wanatofautiana kiviwango, kuna wale wanaofaa kwa ajili ya Mapinduzi Cup, kuna wale wa SportPesa, Kuna wale wa Ligi kuu na kuna wale wa klabu bingwa Afrika.

Kikosi cha Simba kabla ya panga pangua.

Utofauti wa viwango vya wachezaji hawa ni kama mfumo wa elimu wa Tanzania tu, yaani kadri daraja linavyokuwa kubwa ndio idadi ya watu inapungua. Ni vigezo tu ndio vinavyowaweka nje ya daraja fulani la kiuchezaji.

Wachezaji hawa hawajakamilika kwa asilimia 100 lakini wana vitu vingi,vinavyowaongezea uwezo wa kiushindani kuliko wengine.

                                            Meddie Kagere.

Huyu ni Straika kutoka Rwanda mwenye asili ya Uganda.  Ana kasi kubwa anapolikaribia lango la mpinzani, ana nguvu nyingi miguuni kiasi kwamba mashuti yake huwapa tabu magolikipa wengi kuyakamata, usahihi wa pasi zake ni mkubwa, anapenda kumiliki mpira akiwa amezuukwa na wachezaji zaidi ya mmoja, ni mpambanaji akiwa uwanjani. Tangu atue msimbazi hajawahi ripotiwa kukosa nidhamu.

Kagere

Amechezea vilabu 10 tangu mwaka 2004, kabla ya kujiunga na Mnyama akitokea Gor Mahia ya nchini Kenya. Kagere ana uzoefu mkubwa kiasi cha kumfanya awe nunda katika soka la Afrika. Kagere alishawahi kusajiliwa na klabu ya KF Tirana ya Albania huko barani ulaya mwaka 2014 hadi 2015 akitokea Rayon Sports ya Rwanda.

Kagere ni mchezaji ambaye ame-balance, yaani matumizi ya mguu wake wa kulia hayana tofauti kubwa na mguu wa kushoto, pia hana tofauti kubwa na kichwa chake. Ana stamina ya kutosha ya kumsaidia kupasua msitu wa mabeki na kushuti katikati ya miguu ya wachezaji pinzani.

Kagere ana uwezo wa kupambana na mabeki kama Ahmed Fathy,Yasser Ibrahim, Ali Maaloul, Saad Samir, Mahmoud Wahid, Yanick Bangala, Glody Ngonda Muzinga, Botuli  Bompunga na wengine wengi wenye hadhi ya kucheza makundi klabu bingwa Afrika.

                                                 Emmanuel Okwi.

Mshambuliaji Mwiba kutoka Uganda, huyu ndiye mfalme wa muda mrefu kwa timu ya Msimbazi. Ni miongoni mwa mastraika wenye uwezo mkubwa wa kuzifumania nyavu.

Emmanuel Okwi.

Hakuna kinachomsumbua kwenye mechi kubwa, ni ngumu kwake kuzidiwa na presha ya ukubwa wa mechi. Anafanya vizuri akicheza dhidi ya timu ndogo na hata kubwa. Uzuri wake haupo ndani ya Simba pekee bali hata kwa timu yake ya Taifa ya Uganda, kule nako ni mfalme wa mabao na tayari ameshaivusha Uganda katika fainali za AFCON kule Misri.

Amekamilika katika idara nyingi, anatumia vizuri mguu wake wa kulia na kushoto, ana kasi anapokuwa na mpira, anafunga kwa miguu yote na hata kichwa, kiufupi yuko fiti na anaweza kumsumbua beki wa timu yoyote kutoka taifa kubwa Afrika.

                                           Shomari Kapombe.

Ni majeruhi anayeiumiza kichwa klabu ya Simba, huyu ndie beki wa kulia Mtanzania mwenye sifa nyingi za Dan Alves wa Brazil na PSG.

Shomari Kapombe.

Ni beki wa kisasa, anakaba, kulinda na kushambulia kwa wakati mmoja. Ana mapafu ya mbwa, ame-balance, ana stamina ya kutosha, pasi zake za mwisho huwa zina macho.

Ni vigumu kumpokonya mpira akiwa nao mguuni, ana nguvu za kutosha, ni kiraka anayemudu kucheza kama kiungo. Kila timu anayoichezea anakuwa muhimili katika eneo lake. Ni majeruhi pekee ndio kikwazo kwake lakini anaweza kucheza ligi yoyote na kumkaba mshambuliaji yeyote Afrika.

                                                     Jonas Mkude.

“The Stoper” nitaachaje kumtaja wakati ndiye mchezaji wenye stamina kubwa, pasi zake nyingi ni sahihi, ni fundi kwa pasi fupi fupi na ndefu.

Jonas Mkude.

Ana uwezo wa kupiga mashuti nje ya 18 na bado akafunga, miguu yake ina nguvu nyingi, akiwa na mpira kumpokonya ni vigumu kwa kuwa hutumia miguu yake kuulinda, ni mzuri kupokonya mipira kwa mpinzani.

Anafaa katika soka la kiushindani, amecheza muda mrefu na Simba, amecheza mechi nyingi za kiushindani, hivyo presha za mechi kubwa ni rahisi kuzikabili.

Ni kiongozi uwanjani licha kuwa sio nahodha wa timu, ana mchango mkubwa kwa klabu yake katika hatua za mtoano.

Bila shaka ndiye mshika dimba kwa sasa, akizidiwa yeye na timu yote inazidiwa katika maeneo mengi, ubora wake ndio ushindi wa timu. Mkude anafaa kupambana na kiungo yeyote afrika nab ado wakapimana msuli sawa, ubora wa pasi za mwisho na mashuti nje ya 18.

Wakwangu wanne ndio hao, yaani Kagere, Okwi, Kapombe na Mkude. Na wewe andika au ongeza wengine hapo chini ili kwa pamoja tuuende kikosi cha wachezaji 11, wa Simba wanaostahili kucheza hatua ya makundi Klabu bingwa Afrika.

Sambaza....
Subscribe
Notify of

0 Maoni
Inline Feedbacks
Tazama Maoni Yote
0
Tungependa kupata maoni yako, tafadhali tuambiax
()
x