Sambaza....

“…tena natabiri mtachukizwa na wanao watakia mazuri, mtapendezwa na safari za kuelekea kaburi, mtakuwa mazuzu na mtakuwa viburi, wachache mtakumbuka juzuu na zaburi…”

Nimeanza na mashairi ya msanii Kala jeremiah, yeye akitabiri kile kitakachotokea siku za usoni. Ni mahususi kabisa na nia yangu ya kutabiri kile kitakachotokea siku ya jumamosi, januari 12, katika uwanja wa taifa” kwa mchina” pale  Simba SC watakaposhuka dimbani kumvaa mwarabu JS Saoura ya Algeria katika michuano ya klabu bingwa Afrika katika hatua ya makundi ikiwa ni mechi ya kwanza kwa wekundu wa msimbazi katika kundi D.

Kabla sijaenda mbali zaidi ni vema ukanielewa  vizuri kuwa,  utabiri wangu hauhusiani na imani zozote za giza, wala elimu ya unajimu bali ni kile ninachokiona baada ya kuzitazama timu zote mbili katika michezo yao mbalimbali.

Nikianza na wageni JEUNESSE SPORTIVE DE LA SAOURA  , Kwa kifupi unaweza kuiita JS Saoura au JSS. Hii ni klabu inayopatikana Algeria, katika mji wa Meridja katika jimbo la Bechar.

Kikosi cha JS Saoura.

Klabu hii changa ilianzishwa mwaka 2008, rangi kuu za klabu hii ni Njano na Kijani. Uwanja wake wa nyumbani unaitwa Stade 20 Aout 1955 wenye uwezo wa kubeba mashabiki wapatao 20,000 pekee ikiwa ni mara tatu ya uwanja wa taifa wa Dar Es Salaam.

Rais wa klabu hii anafahamika kwa jina la Mohamed Zerouati, huku kocha mkuu wa klabu anaitwa  Nabil Neghiz, ikiwa ni klabu yake ya 11 kuifundisha kama kocha. Kocha huyu anakuwa ni kocha wa 21 tangu klabu hiyo kuanzishwa mwaka 2008.

JS Saoura inashiriki ligi kuu nchini Algeria inayofahamika kwa jina la Ligue Professionnelle 1, na kumaliza katika nafasi ya pili katika msimu ulioisha wa 2017/2018 na kuwafanya washiriki Klabu Bingwa Afrika.

Katika hatua ya awali ya mashindano haya , JS Saoura ilicheza dhidi ya SC Gagnoa ya Ivory Coast, na kuichapa jumla ya magoli 2-0. Mechi ya kwanza JS Saoura iliibuka na ushindi wa 2-0 uwanja wa nyumbani na ugenini walitoka sare tasa. Mechi ya raundi ya kwanza JS Saoura ilicheza na Ittihad Tanger ya Morocco, bila shaka unaikumbuka timu hii ndio ilicheza mchezo wa kirafiki na Simba ikiwa nchini Uturuki. Tanger walikubali kulala kwa jumla ya magoli 2-1, mchezo wa nyumbani walishinda 2-0 na ugenini walifungwa 0-1 na kuwafanya wasonge mbele kwa tofauti hiyo.

Mpaka JS Saoura inaingia katika hatua ya makundi ikiwa na jumla ya goli 4 wao wakiruhusu goli 1 pekee ugenini. Hawajawahi fungwa wakiwa uwanja wao wa nyumbani katika mashindano haya.

Magoli hayo manne yamefungwa na Hammia  goli 2 (kwa penati), Boulaouidet 1 (penati) na  Konate 1.katika michezo yote minne ya hatua ya awali na ya kwanza.

Kwa takwimu hizi haraka haraka nabaini kitu, kwanza JS Saoura wanaonekana hawana safu kali ya ushambuliaji, pili wana safu nzuri ya ulinzi, tatu  wanacheza kwa mipango kutokana na uhitaji wa mechi.

Kwa takwimu hizo hizo pia nabaini kuwa, JS Saoura hucheza mechi za ugenini wakitafuta sare, yaani kama ni alama wanajiwekea basi sare ni asilimia 60, kushinda ni 10, na kufungwa 30, kwanini 30? Kwa sababu wanajua wakitufunga kwao, tutawafunga kwetu. Watacheza huku wakiwa makini kutowaruhusu Simba kuwafunga. Lengo hili huwa wanalifanikisha kwa njia mbalimbali ikiwemo kupoteza muda kwa kujiangusha, kulinda “kupaki basi” na kushambulia kwa kushitukiza. Na mara nyingi mbinu zao hufanikiwa kwa kiwango kikubwa.

Kama ulikuwa hujui, JS Saoura ina jumla ya wachezaji 26 pekee wenye wastani wa miaka 27.5 ukilinganisha na Simba wenye wastani wa miaka 25.6. Wastani huu bila shaka unakuongezea kitu hasa katika suala la uzoefu katika soka na mashindano mbalimbali, maana yake JS ina viongozi wengi uwanjani na  kati ya hao, wachezaji kutoka nje ya Algeria ni watatu, ambayo ni sawa na 11.5% pekee ya kikosi kizima, hii huenda ikamaanisha kuwa na falsafa iliyokomaa yaani hata soka wanalocheza ni soka la nyumbani.

Katika mechi yao ya mwisho ugenini dhidi ya Tanger, walitumia mfumo wa 4-5-1. Mfumo huu una maana kubwa sana kwa timu kama JS Saoura, katika mfumo huu, viungo ndio waamuzi wa mechi, kwani huwa wana kazi kubwa ya kulimiliki dimba na kuhakikisha timu pinzani hawatengenezi nafasi za wazi za kupata goli. Mfumo huu hutumiwa hasa zaidi na timu dhaifu mbele ya timu imara ili kuziba mawasiliana kati ya viungo na washambuliaji wa timu pinzani.

Mfumo huo ndio uliomfunika Clatus Chama, kule Zambia dhidi ya Nkana Red Devils, na kuifanya Simba ilale kwa goli 2-1. Nkana walitumia 4-5-1 kushambulia lakini JS Saoura watautumia kujilinda. Na kikosi JS Saoura kilichoanza dhidi ta Tanger kilikuwa na wachezaji wafuatao:

Nateche alianza golini akiwa pia kama nahodha, beki wa kulia Khoualed, kushoto Bekakchi, wa kati ni Boubekeur na Talah. Viungo wawili wakabaji, Merbah na Bouchiba na mmoja akishambulia ambaye ni Hammia. Viungo wa pembeni (mawinga) kulia alianza Zaidi na kushoto alikuwepo Koulkheir, na mshambuliaji wa mwisho alikuwa ni Boulaouidet.

Katika benchi walikuwepo wachezaji saba ambao ni golikipa Khaled Bookacem, mabeki, El Hadji Youssoupha Konate na Ahmida Zenasni, Viungo Sid Ahmed Aouedj, Nabil Bousmaha, na Yahia Cherif na mshambuliaji Moustapha Djallit.

Katika kikosi chote cha JS Saoura, akiwemo Mtanzania, Thomas Ulimwengu, hakuna mchezaji aliyefunga zaidi ya goli 5 katika msimu huu wa ligi nchini Algeria. Anayeongoza kwa magoli klabuni hapo ni M. Hammia (Kiungo mshambuliaji) ana goli 4, M. Boulaouidet na M. Djallit( washambuliaji) magoli 3, H. Zaidi (winga wa kushoto) goli 2, E. Konate, beki kutoka Ghana ana magoli 2.

Ukiwaangalia wafungaji wa magoli hayo na maeneo wanayocheza utabaini kuwa timu hii haina mfungaji rasmi. Safu yake ya kiungo inaonekana ndio hatari zaidi, ikifuatiwa na ushambuliaji. Pia mabeki wao wanaonekana wanatabia za kupandisha mashambulizi na kucheza vichwa na wakati mwingine kupata magoli kwa njia za kona.

Kwa upande wa Simba, mambo yanaonekana sio mabaya kiasi cha kuyakatia tamaa, kwani hadi Simba inafika katika hatua hii, imecheza mechi 4, imeshinda 3 na kupoteza 1. Imefanikiwa kufunga magoli 12, imefungwa magoli 4 hii ni sawa na tofauti ya magoli 8 sawa na asilimia 73.7 ukilinganisha na tofauti ya magoli dhidi ya JS Saura yenye magoli 3, sawa na asilimia 27.2 pekee.

kikosi cha Simba Sc kikipasha.

Katika magoli yote 12 ya Simba katika michuano hii, magoli 7 yamefungwa na washambuliaji ikiwa ni asilimia 58.3, na magoli 5 yametiwa kimyani na viungo, hii ni sawa na asilimia 41.7.

Ujumla wa takwimu hizi za Simba ukilinganisha na zile za JS Saura utabaini kuwa Simba ina safu nzuri ya Ushambuliaji na kiungo imara chenye uwezo wa kutoa pasi za mwisho na hata kufunga.

Simba inaonekana kuwa imara zaidi katika maeneo hayo mawili. Eneo la ulinzi limeruhusu goli 3 pekee, kitakwimu ukilitazama hili ni sawa na kusema safu ya ulinzi imechangia 20%, kiungo 33% na safu ya ushambuliaji 47% ya ushindi wa Simba katika mechi zote nne kwa kigezo cha magoli ya kufunga na kufungwa.

NAIONA MECHI ITAKUWA HIVI..

Kwanza, Kwa sababu ya uenyeji, Simba watahitaji kushambulia kwa kasi, katika dakika za mwanzoni, yaani kuanzia dakika ya 1-20, huku JS Saura wakijaribu kujilinda kwa kuwatazama Simba wanataka kufanya nini. Katika kitu ambacho watajitahidi waarabu ni kuepuka kufungwa goli la mapema, maana litawachanya na kuwatia wazimu.

Pili, huwezi amini lakini endapo Simba watapata goli la mapema, kuanzia dakika ya 1-20, JS Saura watajilipua, wataanza kucheza kwa jitihada zote yaani kufa na kupona ili wapate sare kwa mechi ya ugenini. Kama wazo lao ni kutafuta japo sare ugenini basi wataitafuta sare hiyo, iwe ya kutofungana au kufungana lakini lazima iitwe sare.

Tatu, JS Saura watajaza viungo wengi katikati lengo ni kutowaruhusu Simba kutawala eneo hilo na kutengeneza nafasi za wazi, hivyo nauona mfumo wa 4-5-1 ukitumika dhidi ya Simba ugenini ili kusaka matokeo. Wataanza mchezo taratibu kwa kuwasoma Simba ili kubaini eneo lenye ufa ili walitumie kupata matokeo.

Nne, nakiona kikosi kilekile kilichocheza dhidi ya Nkana uwanja wa taifa kitajirudia dhidi ya JS Saura, mabadiliko yakiwa ni machache hasa katika eneo la ulinzi kutokana na majeraha ya kiraka Erasto nyoni.

Tano, naiona Simba ikihaha kutoboa tundu katika ukuta wa mabeki wanne wakiungana na viungo wakabaji wawili wa JS Saura na kuifanya mechi hiyo kuwa kama ile dhidi ya KMKM ya Zanzibar katika kombe la mapinduzi.

Sita, natarajia kuyaona maingizo mapya katika benchi la Simba akiwemo kiungo Mrwanda, Haruna Niyonzima, Asante Kwasi na Mohamedi Ibrahim wakipata nafasi katika mechi hiyo.

Haruna Niyonzima, moja wa wachezaji wa klabu ya Simba, katika nafasi ya kiungo.

UTABIRI WANGU.

“ You’ll Never Walk Alone” “ You’ll Never Walk Alone” “ You’ll Never Walk Alone” Mwaka 2005, bila shaka ni mwaka ambao si rahisi kusahaulika hasa kwa mashabiki wa Liverpool.

Katika fainali za Klabu Bingwa Barani ulaya, mwaka huu unakumbukwa kama mwaka wa maajabu, yaani “the miracle of Instanbul”

Kwanini ni maajabu, kwanza fikiria kuhusu Liverpool kushindwa kufika fainali tangu miaka ya 80, na ikiwa inalinyemelea taji lake la 5, kipindi cha kwanza tu ubao ulisomeka 3-0, AC Milan ikiongoza

Kipindi cha mapumziko, mashabiki walitumia nguvu yao kama mchezaji wa kumi na mbili kwa kuimba kwa hisia kali “ You’ll Never Walk Alone”.

Kipindi cha pili kilianza, ndani ya dakika 6, Liverpool ilirudisha magoli yote matatu na ubao kusomeka 3-3, shukrani zimuendee, Gerrard 54’,Smicer 56’ na Xabi Alonso 60’. Mtanange huo ulilazimika kumalizika kwa mikwaju ya penati, shukrani za dhati kwa golikipa Jerzy Dudek kwa kudaka mikwaju ya wakali Andrea Pirlo na Andriy Shevchenko na kuwafanya Majogoo wa jiji kubeba ndoo yao ya tano.

Hadi kufikia hatua hii naamini kuwa shabiki ana mchango mkubwa katika matokeo ya timu, unakumbuka mchezo wa mwisho wa mashindano haya Simba walijaza uwanja, na Nkana walikula 3-1. Endapo kama Mashabiki watakubali wito na kujaa, Simba itashinda.

Idadi kubwa ya Mashabiki wa Simba SC waliojitokeza dhidi ya Nkana Red Devils, klabu bingwa barani Afrika katika uwanja wa Taifa wa Dar es Salaam.

Wachezaji wa Simba wakiwa fiti, yaani wakiwa katika viwango vyao tunavyovijua, wakiwa wapo makini katika kushambulia na kuokoa, Simba itashinda.

Kwa jinsi nilivyokuelezea hapo juu, najua mchezo utakuwa mgumu lakini pia naamini Simba hawatofanya makosa mengi ya kuwagharimu.

Mwisho kabisa, natabiri nikiwa kama na-bet, Simba itaibuka na ushindi wa goli 2-1.   Je wewe unatabiri nini kwenye huu mchezo?

Sambaza....