Stephen Aziz Ki
Uhamisho

Aziz ki ni kama Ronaldo tuu Yanga!

Sambaza....

Stephane Azizi Ki Kama simulizi yake ni kweli basi yawezekana ndiye mchezaji mwenye thamani kubwa nchi Tanzania kwa sasa akitajwa kuwagharimu nusu bilioni klabu yake mpya ya Yanga.

Si hapo tu inaaminika maslahi yake yamepangwa yakapangika vizuri kuanzia mshahara na bonansi zake ndani ya Yanga.

Swali la msingi ni kwamba kuwa mchezaji wa kipekee mwenye maslahi bora ya zaidi ndani ya kikosi inaweza kuharibu umoja na ushirikiano wa kitimu?.

Mimi siamini hilo kwenye mpira wa kulipwa, ndio yawezekana hatupo kwenye ligi ya kulipwa kiuhalisia lakini tendo la kusaini mikataba ni kwamba tupo ndani yake.

Kwenye ‘Professional football ‘ tabaka la malipo lipo wazi na linatambulika miongoni mwa wachezaji wa timu hiyo, yawezekana mwingine akalipwa hadi mara tano ya mchezaji mwingine lakini mambo yakaenda.

Kwenye mpira wa ridhaa kuwa na tabaka la malipo miongoni mwa wachezaji ni kutengeneza tabaka ambalo hupelekea ‘kisununu ‘ au roho ya korosho miongoni mwa wachezaji madhara yake ni timu kutokufanya vyema.

Cristiano Ronaldo.

Kwenye mpira wa kulipwa hilo halina nafasi ndiyo maana unakuta pale Manchester United Ronaldo analipwa paundi laki tano na ushee ambazo ni juu ya bilioni moja kwa wiki huku mchezaji kama Mc Tomminay analipwa paundi elfu 20 sawa na takribani milion 50 tu kwa juma moja.

Azizi Ki angekuwa amekuja zama zile ngumu soka letu halijaingia katika uweledi huu hivyo haiwezi kuathiri chochote.

Kwenye eneo la kiufundi Azizi Ki kwa kile alichokionesha kwenye michuano ya Kombe Shirikisho tuliona kitu kikubwa sana na kama atakiamishia kwenye timu yake mpya kiukweli atakuwa wamelamba dume.

Yeye binafsi hana shaka anakuja kuingia kwenye mfumo wowote wa timu Nabi atakayotaka kutumia mfano 4-2-3-1, 4-3-3, 3-5-2 Ki ana nafasi ya kucheza.

Stephen Aziz Ki.

Alipokuwa Asec Mimosa alitengeneza ushirikiano mzuri uliokuwa na faida na Karim Konante ambaye kiuchezaji anafanana sana Fiston Mayele hivyo basi anaweza kupata pacha mwingine akaweza kushine tena.

Nabi atakuwa na maamuzi mbalimbali ya kumtumia kwa kuwa Ki anamudu vyema nafasi zote za ushambuliaji wa kati na ule wa kutokea pembeni pande zote mbili.

Simuoni kwenye benchi kwa hali yeyote ile kutokana na uwezo wake wa kiuchezaji silaha yake kubwa ikiwa kasi na maamuzi sahihi kwa wakati sahihi.


Sambaza....
Tafadhali tumia viungo vya mitandao ya jamii kusambaza.