John Bocco vs Al-Ahly
EPLLigi KuuMabingwa Afrika

Tunambeza, tunamlaumu na bado tunamtegemea, John Romelu Raphael Lukaku Bocco.

Sambaza....

Ukiachana na Marc Wilmots, Paul Van Himst, Benard Voorhoof anayefuata sio Edin Hazard wa Chelsea bali ni mtu mwenye miraba minne, anamiliki uzito wa kilo 94, na urefu wa 1.9m sawa na futi 6 na inchi 3, tangu mwaka 2010 hadi leo ameifungia timu yake ya taifa magoli 45 katika mechi 79 alizocheza na kuwa mfungaji bora wa muda wote.

Gharama za  uhamisho wake kutoka Everton mwaka 2017 zilikuwa ni Euro milioni 85.  Ukiachana na Neymar, Ronaldo, Mbappe na yeye yupo 10 bora kwa gharama kubwa za usajili. Huyu ndie Romelu Menama Lukaku Bolingoli.

Amechezea vilabu vingi kabla ya kutua Old Traford. Alishawahi kukiwasha na Chelsea miaka ya 2011-2014 lakini mwaka 2012 akiwa Chelsea alipelekwa kwa mkopo  West Bromwich Albion, akicheza mechi 35 akifunga magoli 17, kisha akapelekwa kwa mkopo Everton mwaka 2013 kabla ya kununuliwa jumla jumla mwaka 2014-2017 na hapo ndipo ufalme wa Lukaku ukaonekana.

Ameifungia Everton magoli 53, katika mechi 110 alizocheza, na hiki ndicho kilichomshawishi Mreno Jose Mourinho kuona ni mtu sahihi kwa timu kubwa kama Manchester United, na tayari ameshaichezea Man U mechi 60 na kuifungia magoli 28.

Katika ligi kuu nchini Uingereza, EPL Lukaku tayari amesha weka kambani magoli 12 na kumuweka nafasi sawa na Edin Hazard wa Chelsea, Raheem Sterling wa mana city na Alexandre Lacazette wa Arsenal.

Lukaku ni miongoni mwa wachezaji wa Man U wanaotamkwa sana midomoni mwa mashabiki na wadau wa soka duniani, si kwa uzuri kama anavyosemwa Paul Pogba bali ni kwa ubaya hasa wa kubeza kiwango chake, wengine wakisema amenenepa bila mpango. Kila mtu ana lake la kusema.

Hivi majuzi Man U ilimrarua Southampton na Lukaku alizisabahi nyavu za Southampton mara mbili, mashabiki wa Man U walijawa na furaha na kusahau kuwa Lukaku ana kilo 94.

Lukaku ameshacheza dakika  1694, amefunga magoli 12, sawa na goli 1 kwa kila dakika 141, sawa na mechi mbili kasoro dakika 39 mpira kumalizika.  Na amepiga mashuti 38, asilimia  74 ya mashuti yake yamelenga lango.

Lukaku

Tafsiri ya takwimu hizi ni kwamba, Lukaku amefunga magoli 12 pekee katika nafasi 38 alizopata za kupiga shuti. Wastani wa ufungaji wake ni sawa na kucheza mechi moja  na dakika 51. Kumbe ndio maana tunamlaumu, tunambeza na bado akifunga tunamsifu hii ni dalili kuwa  tunamtegemea.

Masikini JOHN BOCCO  naye kaingia kwenye mtego sawa na wa Lukaku. Au sijui kwa sababu wote ni WEKUNDU! Bocco naye anasemwa sanaa, tena na mashabiki wa timu yake na hata upande wa pili. Wengi wanasema ameshachoka, akipata nafasi 6 za wazi anatumia 2 lakini akifunga utasikia tu” huyo ndio PAPA JOHN BOCCO” yaani huitwa majina yote ya kumsifia.

Kwa mwezi Februari pekee Bocco amefunga goli 4 sawa na Salimu Aiyee wa Mwadui fc, amewapiga “gap” Ayubu Lyanga wa Coastal na Salumu Mashaka Kimenya wa Prisons wenye goli 2 na 1 mtawalia. Lakini amepitwa na Meddie Kagere mwenye  goli 5.

Nani asiyejua kama Bocco ndiye aliyetoa pasi ya goli la Meddie Kagere dhidi ya Mwarabu Al-Ahly uwanja wa taifa? Vipi dhidi ya mahasimu wao Yanga? Alitoa pasi ya mwisho pia. Hakuishia hapo , mechi iliyofuata alifunga magoli mawili dhidi ya African Lyon kule Arusha.

Dhidi ya Azam alifunga goli, katika ushindi wa 3-1. Dhidi ya Stendi United tena anafunga goli 2. Kwa mantiki hiyo Bocco amehusika matika mechi 5 mfululizo. Lakini bado anabezwa, si na mashabiki wa upande wa pili na hata mashabiki wa Simba.

Ukiachana na hayo yote, Bocco ana rekodi nyingi zinazombeba kuwa mchezaji mkubwa. Idadi kubwa ya magoli ligi kuu Tanzania bara anayo yeye, yeye ndiye mfungaji bora wa muda wote, anagoli zaidi ya 100. Mchezaji aliyezifunga goli nyingi timu za Simba na Yanga rekodi pia anayo yeye. Ni mchezaji bora wa msimu uliopita. Na ni kepteni wa timu kubwa kama Simba.  Bado unamchukulia poa tu?.

Mara zote amekuwa akikiri kukosa mabao mengi tu awapo uwanjani, mfano ni mechi dhidi ya Mwadui, alikosa nafasi 3 za wazi. Kushindwa kubadili nafasi kuwa goli ni sehemu ya sifa ya Straika, kuna wakati anakosa na kuna wakati  anazitumia hata zile unazoziona sio nafasi za goli, mfano ni goli alilofunga dhidi ya Prinsons kule Mbeya msimu uliopita. Alifanya “fantastic turn” na kufunga bao la kideo.

Ni huyu huyu Bocco mfalme wa Azam wa muda wote, timu ilianzia mikononi mwake, na hata baada ya yeye kuondoka akiwa na marafiki zake  Shomari Kapombe, Aishi manula na Erasto Nyoni Azam nayo imeisha makali yake, sio Azam ile ya John bocco na Joseph Omog.

Bocco akiwa Azam Fc, alifunga mabao 84

Kiufundi Bocco hufanya nini uwanjani?

Mechi tano za hivi karibuni kama hajafunga basi atakuwa ametoa pasi ya goli. Unadhani kwanini Bocco akiwa fiti huwa haanzii benchi ukilinganisha na Kagere na Emmanuel Okwi? Bocco ni mpambanaji, ni kiongozi ndani ya uwanja . Thamani ya yeye kucheza hata asipo funga ni kubwa.

Bocco huhitaji nafasi ndogo kupiga shuti, mipira ya juu yote ni uhakika kuchezwa na kichwa cha Bocco. Hii inatoa uwanda mpana kwa timu kushambulia chini na juu kwa wakati mmoja. Bocco ni mkabaji, hukaba kuanzia eneo la juu la timu pinzani. Timu ikizidiwa eneo la kati itakuwa na uwezo wa kupiga mipira mirefu ya juu kwa sababu yupo mpokeaji wa mipira hiyo. Kimo kinamuunga mkono.

Bocco hukaa juu kama straika wa pembeni ya Kagere, yaani Bocco humzunguuka Kagere muda wote akihaha kushuka chini kulia na kushoto kupokea mipira, huku Kagere akibaki kama straika wa mwisho, ili asiliache eneo la mabeki wa kati wazi, asiwafanye watoke kwenda kushambulia.

Bocco humsaidia Kagere kubaki eneo la juu, na kuwafanya mabeki wasipandishe timu.Bila Bocco, Kagere angekuwa anahaha kushoto na kulia na matokeo yake eneo la mabeki wa kati wa timu pinzani linakuwa halina hatari yoyote. Na hiki ndicho kilichotokea dhidi ya AS Club Vita, athari yake ni Simba kula tano.

Hadi kufikia hapa bado unambeza tu Bocco? Huenda ulikuwa humjui vizuri anafanya nini nje na ndani ya uwanja, huenda ulikuwa hujui rekodi zake, huenda ulikuwa hujui ukubwa wa Bocco nje ya Simba. Sasa utakuwa unajua, bado utamchukulia poa tu Bocco? Umesahau penati yake dhidi ya Nkana, Kitwe Zambia ilizaa goli lililoipa ahueni Simba ya kushinda uwanja wa taifa?

Lukaku na Bocco hawa ndio wapo tayari kutoa jasho na damu zao kwa ajili ya timu zao  ndio maana hata hawashughulishwi na kusemwa na mashabiki wala vyombo vya habari. Kiukweli “ tunawabeza machoni lakini tunawategemea mioyoni”.

Sambaza....
Subscribe
Notify of

0 Maoni
Inline Feedbacks
Tazama Maoni Yote
0
Tungependa kupata maoni yako, tafadhali tuambiax
()
x